MABADILIKO SERIKALINI: Rais atuliza joto la kutimua baadhi ya mawaziri
WANDERI KAMAU NA WINNIE ATIENO
RAIS Uhuru Kenyatta ameondoa hofu ya uwezekano wa mabadiliko ya baraza la mawaziri ambayo imekuwepo nchini kwa muda sasa.
Hilo limechangiwa na sakata za ufisadi ambazo zinawaandama mawaziri kadhaa, hali ambayo imeibua uwezekano wa mabadiliko serikalini.
Lakini akihutubu Jumanne kwenye Kongamano la Wakuu wa Shule za Upili Barani Afrika, jijini Mombasa, Rais alitaja madai hayo kama uvumi usio na msingi wowote.
“Watu wamekuwa wakieneza uvumi kuhusu uwepo wangu hapa Mombasa kwa majuma mawili. Nimeamua kurudi Nairobi ili kuondoa wasiwasi huo,” akasema.
Baadhi ya mawaziri waliripotiwa kujawa na hofu ya kuhamishwa ama kuondolewa katika nyadhifa zao, hasa habari zilipoobuka Jumatatu kwamba rais angetangaza baraza jipya la mawaziri.
Ilimbidi Kaimu Msemaji wa Ikulu Kanze Dena kujitokeza kukanusha madai hayo.
“Hatufahamu mipango ya mabadiliko yoyote ya mawaziri. Ikiwa ingekuwepo, rais mwenyewe angekuwa ameieleza nchi,” akasema Bi Dena.
Baadhi ya sababu zilizokuwa zikidaiwa kumsukuma rais kufanya mageuzi hayo ni kuibuka kwa misururu ya sakata za ufisadi zinazowakumba baadhi ya mawaziri wake, hali inayotajwa kupaka tope juhudi zinazoendelea za kukabiliana na ufisadi.
Miongoni mwa sakata hizo ni utata wa uagizaji wa sukari yenye sumu nchini, sakata ya ununuzi wa shamba la Ruaraka jijini Nairobi, kashfa ya uhaba wa mahindi miongoni mwa zingine.
Katika sakata ya sukari, ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Biashara imependekeza kuchukuliwa hatua kwa mawaziri Henry Rotich (Fedha), Aden Mohamed (Masuala ya Afrika Mashariki) na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Willy Bett kwa kutowajibika.
Mawaziri Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani), Amina Mohamed (Elimu), maafisa wa juu wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kati ya maafisa wengine wakuu serikalini pia wamejipata lawamani kutokana na sakata tata ya ununuzi wa ardhi ya Ruaraka.
Jana, baadhi ya wabunge walieleza kuwepo kwa shinikizo “kutoka juu” kutopendekeza kuchukuliwa hatua kwa mawaziri Rotich na Aden kwa kupitisha ripoti kuhusu sukari hiyo tata.
Mbunge wa Dagoretti Kaskazini alithibitisha kwamba kuna shinikizo hizo, alizodai zinatoka kwa watu maarufu ambao alikataa kuwataja.
“Kuna watu wengi wanaotaka ripoti hii kubadilishwa. Kuna mipango ya kichinichini inayoendelea kuhakikisha ripoti hii inakataliwa Bungeni,” akasema Bw Arati.
Akiwa Pwani, Rais alikutana faraghani na Kiongozi wa ODM Raila Odinga hali iliyoongeza hofu za mageuzi serikalini.
Wiki iliyopita, kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka pia alitangaza kuiunga mkono serikali ya Jubilee, akiahidi kushirikiana nayo kwa manufaa ya nchi.