Mabunda ya Sh1m yapatikana kwa buti ya gari la kaunti mpakani
NA MWANDISHI WETU
POLISI Jumapili wamenasa dereva wa Kaunti ya Samburu akisafirisha mabunda ya fedha, siku moja baada ya Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Patrick Njoroge kuwataka Wakenya kubadilisha noti za 1,000 kabla ya Oktoba 1, mwaka huu.
Dereva huyo aliyekuwa akiendesha gari lenye nambari za usajili 25CG 032A, alikamatwa katika kizuizi cha Learata kwenye barabara ya Isiolo-Moyale, karibu na mpaka wa Kenya na Ethiopia.
Lejisaat Samuel Supuko, 38, ambaye ni dereva katika wizara ya huduma za jamii ya Serikali ya Kaunti ya Samburu, alipatikana akiwa amebeba Sh 1,099,000 tasilimu katika buti ya gari alilokuwa akiliendesha.
Kulingana na polisi, mshukiwa hakuweza kufichua chanzo cha fedha hizo na wala hakusema alichokuwa akienda kuzifanyia.
Haijulikani ikiwa fedha hizo zilikuwa za mshukiwa alikuwa ametumwa na wakubwa wake.
Wakati wa maadhimisho ya sherehe za Madaraka, Jumamosi, Gavana wa CBK Njoroge alisema kuwa noti za Sh1000 zinazotumika sasa zitakosa kazi kuanzia Oktoba 1 na akawataka walio na hela hizo kuzibadilisha.
Dkt Njoroge alisema hatua hiyo itasababisha hela zilizofichwa na wafisadi nyumbani kukosa kazi.