Madaraka Dei yahamishiwa Homa Bay sababu ya ‘masharti makali’ ya viongozi Kitui
MAADHIMISHO ya siku ya Madaraka Dei ya mwaka wa 2025 itafanyika katika Kaunti ya Homa Bay.
Hii ni kulingana na tangazo lililotolewa na Katibu katika Wizara ya Mambo ya Ndani Raymond Omollo.
Hapo awali, eneo la Ziwa lilipaswa kuandaa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ya Oktoba 20, 2025 na hii ingeipa kaunti husika miezi minane kujitayarisha.
Rais William Ruto alitangaza hayo alipozuru Kaunti ya Homa Bay mnamo Februari mwaka jana wakati wa kongamano la pili la kimataifa la uwekezaji katika kaunti hiyo.
Hii ni baada ya Gavana Gladys Wanga kumwomba Rais aruhusu kaunti hiyo kuandaa likizo ya kitaifa.
Lakini hii ilibadilishwa na tangazo likatolewa Alhamisi.
Mpango wa awali ulikuwa Kaunti ya Kitui itumike kama mahali pa kuadhimisha Siku ya Madaraka 2025.
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Seneta wa Kitui Enoch Wambua walikuwa wametoa masharti makali kwa Rais Ruto kabla afike kuongoza sherehe hiyo.
Kalonzo alimtaka Ruto kukamilisha barabara ya Kibwezi-Kitui huku Wambua akitaka kiongozi wa nchi aombe radhi kwa “kuita jamii ya Wakamba wakulima wa ndengu”.
Sasa kaunti hiyo itaandaa Mashujaa Dei baadaye Oktoba.
Viongozi wanaoandaa sherehe za kitaifa sasa wana miezi mitatu pekee ya kuandaa Uwanja wa Raila Odinga ulioko katika Mji wa Homa Bay kwa siku hiyo.
Dkt Omollo alisema mada ya Siku ya Madaraka ya mwaka huu ni kuhusu uchumi wa baharini, na Homa Bay patakuwa mahali pazuri ambapo hafla hiyo inaweza kuandaliwa.
Kaunti hiyo ina mojawapo ya fuo ndefu zaidi katika Ziwa Victoria.
Serikali pia inatekeleza miradi muhimu ya maendeleo ndani ya kaunti hiyo ambayo itasaidia kufufua uchumi.
Miongoni mwa miradi hiyoni kukarabati gati (pier) katika miji wa Homa Bay, Kendu Bay, Mbita na Sena katika Kisiwa cha Mfangano.
Akizungumza wakati wa kukagua eneo la hafla hiyo, Dkt Omollo alitoa wito kwa wakazi wa Homa Bay, hasa wafanyabiashara kutumia fursa ya siku hiyo kujipa riziki.