HabariSiasa

Madiwani waapa kupambana na Gavana Waiguru

June 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

UAMUZI wa maseneta kuunda kamati maalumu ya kuamua hatima ya Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru, umeibua hasira miongoni mwa mahasimu wake wa kisiasa.

Mnamo Jumanne, maseneta 45 walipiga kura kukubali kamati iundwe, tofauti na 14 ambao walipendekeza kikao kizima cha Seneti kikae kumhoji Bi Waiguru kuhusu madai yaliyotolewa dhidi yake na madiwani wa Kirinyaga wanaotaka abanduke.

Jana, madiwani 23 wa Kirinyaga wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika bunge la kaunti hiyo, Bw Kamau Murango walisema hata kama Seneti itamwokoa Bi Waiguru, watapambana naye mashinani.

Wanahofia kuwa huenda hakutakuwa na uamuzi wa haki katika kamati.

“Tuliudhika sana. Sisi hatutafanya kazi na gavana ambaye anakaidi bunge la kaunti kila mara na anayekiuka sheria,” akasema.

Aliyeandaa mswada wa kumng’atua Bi Waiguru katika bunge la Kirinyaga, Kinyua wa Wangui alitaja matukio ya Seneti kama “ukora na unafiki.”

“Ni wazi kumeandaliwa njama ya kutupuuza kama bunge la Kaunti na Uhuru na Raila wanafaa waelewe kuwa hata wakimwokoa Waiguru katika Seneti, bado atakuja hapa Kirinyaga na tutawafunza adabu za kutuheshimu,” akasema.

Kiongozi wa Chama cha Narc-Kenya, Bi Martha Karua alisema imebainika wazi hakuna uwezekano wa ushirikano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwafaa Wakenya katika vita dhidi ya ufisadi na maovu mengine ya kiutawala.

“Kwa sasa ni wazi kuwa hata wao ni visiki katika vita dhidi ya ufisadi,” akasema.

Hata hivyo, kamati maalumu ambayo itasimamiwa na Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala, ilisisitiza itatenda haki katika maamuzi yake.

Baada ya kuchaguliwa jana kuongoza kamati hiyo, Bw Malala alisema hatima ya Bi Waiguru itajulikana Ijumaa wiki ijayo watakapowasilisha ripoti kwa Seneti.

Malala alisema wawakilishi wa bunge la kaunti ya Kirinyaga watawasilisha ushahidi wao mbele ya kama hiyo Jumanne.

Kisha Jumatano Gavana Waiguru atafika mbele ya kamati hiyo ya wanachama 11 kujitetea kabla ya kamati hiyo kufanya kikao cha faragha kuandaa ripoti yake ya mwisho.

“Tunafahamu fika kwamba suala hili limefuatiliwa kwa makini na Wakenya wote; kando na watu wa Kirinyaga. Kwa hivyo, tunawahakikishia kuwa tutaendesha kazi hii kwa haki na uwazi. Pande zote husika zitapewa muda tosha wa kutetemea misimamo yao mbele yetu,” akasema Seneta huyo wa ODM ambaye ni naibu kiongozi wa wachache katika Seneti.

Seneta Maalum Abshiro Halake (Kanu) alichaguliwa kuwa naibu mwenyekiti baada ya kumbwaga Seneta wa Nyandarua Mwangi Githiomi.

Kufikia sasa, Bi Waiguru amepata utetezi kutoka kwa Chama cha ODM, serikali kuu kupitia kwa Waziri wa Utumishi wa Umma Profesa Margaret Kobia, na viongozi wengine wenye ushawishi kama vile Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli.

Ikiwa Kamati iliyobuniwa itabaini kuwa mashtaka dhidi ya Gavana Waiguru yana mashiko, itaandaa ripoti na kuiwasilisha kwa kamati ya maseneti wote ili ijadiliwe.

Na ikiwa angalau wanachama sita wa kamati hiyo watatupilia mbali tuhuma dhidi ya Gavana Waiguru, suala hilo litakomea hapo. Hata hivyo, ripoti itawasilisha kwa Seneti kwa ajili ya rekodi pekee.

Ripoti za George Munene, Charles Wasonga na Mwangi Muiruri