Maelfu ya Shule hatarini kufungwa
MPITO kutoka Sekondari msingi hadi Sekondari Pevu umeanza kuibua changamoto kubwa katika shule za upili za umma nchini Kenya, huku idadi kubwa ya shule ndogo zikikabiliwa na hatari ya kufungwa.
Shule kubwa na zenye hadhi ya kitaifa zinaangamiza shule ndogo za ngazi ya chini, na yote haya yanahusiana na idadi ya wanafunzi.
Shule za upili zilikuwa na madarasa manne: Kidato cha Kwanza hadi cha nne.
Chini ya Elimu inayozingatia Umilisi (CBE), shule zitakuwa na madarasa matatu tu.
Kwa kuwa hakukuwa na mpito wa wanafunzi kutoka shule za msingi hadi upili tangu 2024, shule za upili sasa zina vidato vya tatu na nne pekee, kumaanisha ni madarasa mawili tu yamejazwa. Hii inasababisha darasa zima kuwa tupu, hata shule zinaposajili wanafunzi wa Gredi 10 mwaka huu.
Kwa kuwa bado kuna nafasi ya darasa zima, shule yoyote inaweza kusajili mara mbili ya wanafunzi waliokuwa wakiwasajiliwa awali. Hii imetoa faida kwa shule kubwa, huku wazazi wakiamua kupeleka wanao shule zenye hadhi kubwa badala ya shule walizoteuliwa wanafunzi wao. Matokeo yake ni baadhi ya shule kuzidiwa na wanafunzi, huku nyingine zikikosa wanafunzi kabisa.
Hali hii inaweza kuharakisha mchakato wa kufungwa kwa shule ndogo, kulikotangazwa na Wizara ya Elimu mwaka jana. Wizara ilibainisha kuwa shule 2,700 za umma zina idadi ndogo sana ya wanafunzi ikiwa ni chini ya 150 kwa jumla.
Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, alisema shule zilizo na wanafunzi wachache zinachukuliwa kuwa hazina ufanisi, hasa pale shule nyingine nyingi ziliko zikiwa zimejaa.
“Hakuna faida kuwa na shule yenye watoto 10. Tunahitaji shule zenye miundombinu yote na idadi sahihi ya wanafunzi. Hakuna haja ya kuwa na shule 10 mahali ambapo kuna wanafunzi 1,000 huku shule moja ikiwa na watoto 100 pekee,” alisema Bw Ogamba.
Shule ndogo, hasa za kiwango cha kaunti ndogo, zinaendelea vibaya mwaka huu.
Katika Kaunti ya Turkana, Philadelphia Mixed Day Secondary haijapokea mwanafunzi wa Gredi 10 hata mmoja. Mkurugenzi wa shule hiyo, Julius Atieno, alisema shule ilianzishwa 2024 na bado haijapokea wanafunzi. Alitaka msaada kutoka kwa viongozi wa eneo kuwarejesha wanafunzi walioacha shule kutokana na shughuli za uchimbaji wa dhahabu au waliokataa kujiunga na Gredi 10.
Katika Kaunti ya Trans Nzoia, St Paul’s Kapchepsir Secondary School ilipokea wanafunzi wanne tu kati ya 45 waliotarajiwa. Mkurugenzi, Wycliffe Magero, alisema agizo la Rais William Ruto linalohitaji wanafunzi wa Gredi 10 kujiunga na shule bila kujali kama wana karo au sare, linaweza kuokoa wanafunzi wengi walio nje ya shule.
Hali kama hiyo inakumba kaunti za Baringo, Makueni, Kitui, Machakos, Tana River, Homa Bay, Bomet, Nakuru, Kirinyaga, na Busia, ambapo shule ndogo zimekosa wanafunzi au kupokea chini ya nusu ya wanafunzi waliotarajiwa, jambo linaloashiria uwezekano wa kufungwa kwa shule hizi.
Wazazi na walimu wanasema shule ndogo zinaweza kufungwa au kuunganishwa ili kupunguza gharama.
Hali hiyo ni hatari kwa shule ndogo, kwani mgao wa serikali unategemea idadi ya wanafunzi.
Aidha, juhudi za Serikali na viongozi wa shule kushirikisha jamii ili kuhakikisha mpito wa Gredi 10 kwa asilimia 100, zinaendelea, lakini changamoto za kifedha na upendeleo wa shule kubwa bado unatishia maisha ya shule ndogo.
Ripoti za Mercy Simiyu, Flora Koech, Evans Jaola, Barnabas Bii, Sammy Lutta, Jurgen Nambeka, Pius Maundu, George Odiwuor, George Munene, Joseph Openda, Vitalis Kimutai na John Njoroge.