Habari

MAFURIKO: 237 wafa huku 800,000 wakiachwa bila makao

May 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Ugatuzi Eugene Wamalwa amefichua kuwa kufikia Jumatano asubuhi jumla ya watu 237 walikuwa wamefariki maeneo mbalimbali nchini kutokana na mafuriko.

Aliongeza kuwa zaidi ya familia 161,000 (sawa na jumla ya watu 800,000 ) zimeachwa bila makao huku mali ya thamani isiyojulikana ikiharibika.

Alisema huenda idadi hiyo ikapanda kwa sababu mvua ya masika inatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Mei.

Alisema hayo Jumatano kwenye kikao na wanahabari Nairobi baada ya kuzuru kaunti za Nakuru na Narok kukagua hasara iliyosababishwa na janga hilo.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni karibu na Ziwa Victoria, Ziwa Naivasha, Mto Tana, Mto Nzoia na Kati mwa Kenya karibu na mito ambayo huelekeza maji katika Mto Tana kutoka milima ya Aberdares.

“Idadi ya Wakenya ambao wamefariki kutokana na athari za mafuriko ni 237 kufikia sasa, idadi ambayo ni juu zaidi kuliko vifo kutokana na Covid-19. Hii ina maana kuwa hatua madhubuti ni sharti zichukuliwe kuzuia janga hili kando na kuwasaidia wahasiriwa,” Bw Wamalwa akasema.

Alikuwa ameandamana na Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko na Katibu katika Wizara ya Ugatuzi Charles Sunkuli.

Bw Wamalwa alisema serikali na mashirika mengine ya ufadhili, kwa pamoja, wanafadhili mpango wa kusambaza chakula na mahitaji mengi kwa wahasiriwa wa mafuriko kote nchini.

Waziri alitoa wito kwa wahisani wakiwemo wanasiasa ambao wangependa kuwasaidia waathiriwa kufanya hivyo kwa ushirikiano na makamishna wa kaunti na Magavana.

“Hii ndiyo njia ya kuzuia vurugu na mkanyagano wakati wa usambazaji wa chakula,” Bw Wamalwa akasema.