Habari

Mafuriko yasomba makazi ya familia 10,000 Nyando

May 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

ZAIDI ya familia 10,000 katika vijiji vya Kabonyo na Nduru kwenye wadi ya Kabonyo Kanyagwal, eneobunge la Nyando zimesalia bila makao kutokana na mafuriko ambayo yamekumba eneo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Familia hizo sasa zimepiga kambi katika Shule ya Msingi ya Ugwe na kituo cha kibiashara cha Nyang’ande baada ya nyumba zao kusombwa na hata nyingine kuporomoka.

Wengine nao sasa wanaishi kwenye daraja la Pombo lililojengwa na serikali ya Mzee Jomo Kenyatta miaka ya 70 kusaidia kupitisha maji kwenye mashamba ya mpunga.

Aidha soko maarufu la Odega/Omuonyole ambalo lilikuwa makazi kwa baadhi ya walioathirika nalo lilisombombwa Ijumaa usiku na sasa wakazi wanaomba msaada kutoka kwa serikali kupata eneo jingine la kujisitiri.

Mafuriko hayo pia yamesomba kabisa shule ya msingi ya Kandaria.

Vitabu, samani, masjala na madarasa yote yamejaa maji wakati huu shule zimefungwa kutokana na janga la virusi vya corona

Baadhi ya wakazi waliozungumza na ‘Taifa Leo’ walisema kwamba hawajapokea msaada wowote kutoka kwa kaunti, wanasiasa au mashirika ya kijamii.

“Nimeteseka sana tangu wiki jana nilipohama kwangu baada ya kupoteza mali yangu kutokana na mafuriko na tena nimelazimika kuhama baada ya mafuriko kufika hapa sokoni,” akasema mkazi Mary Ocharo.

Mkazi mwengine Collins Ochanjo ambaye amelazimika kuhamia kituo cha kibiashara cha Nyang’ande naye alisema kuna hatari ya mkurupuko wa magonjwa kama kipindupindu na pia corona kwa sababu hali haiwaruhusu kuzingatia maagizo ya Wizara ya Afya ya kuzuia maambukizi zaidi.

“Hapa tuna njaa na watu wanajishughulisha na namna ya kupata chakula badala ya kudumisha maagizo ya corona. Viongozi wetu nao wametusahau na tunaomba kaunti na serikali zitutumie vyakula, neti za kukinga mbu na dawa,” akasema.

Kando na makazi ya watu kusombwa, mafuriko hayo pia yameharibu maelfu ya ekari za mashamba ya mpunga katika wadi hiyo.

Wiki jana, ziara ya Mawaziri Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na Sicily Kariuki (Maji) eneo la Ahero ambalo ni umbali wa kilomita 25 kutoka Kabonyo Kanyagwal haikufanyika kutokana na hali mbaya ya hali ya hewa ambayo haingeruhusu usafiri wa ndege angani.

Aidha suala la mafuriko limezua uhasama mkubwa wa kisiasa kati ya Gavana Profesa Anyang’ Nyong’o na Seneta Fred Outa.

Gavana huyo wiki jana alifurushwa alipopeleka msaada wa vyakula kwa waathiriwa wa mafuriko eneo la Muhoroni.

Bw Outa naye amelamu utawala wa Profesa Nyong’o kwa kuwapuuza wakazi na kutotimiza yale aliyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Mbunge wa Nyando Jared Okello naye ameahidi wakazi kwamba anashirikiana na Bi Kariuki kuhakikisha matuta yamejengwa kwenye mito midogo inayopakana na ule wa Nyando ndipo maji yote yaelekezwe Ziwa Victoria.