Mafuriko yaua watu 285 nchini Kenya
Na SAMMY WAWERU
IDADI ya watu waliofariki kutokana na athari za mafuriko ya mvua inayoshuhudiwa maeneo mbalimbali nchini imefika 285.
Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa amesema idadi hiyo ilithibitishwa kufikia Jumanne jioni.
“Kufikia Jumanne jioni, idadi ya waliokufa maji iliongezeka kutoka 256 tuliyotangaza hapo awali hadi 287,” amesema waziri akihutubu katika makao ya Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa jijini Nairobi leo Jumatano.
Pia amesema idadi ya waathiriwa wa mafuriko imepanda kutoka 808,000 hadi 810,655.
Kwa kipindi cha muda wa miezi miwili iliyopita, maeneo tofauti nchini yamekuwa yakishuhudia mvua kubwa ambayo kando na kusababisha maafa na maelfu kuachwa bila makao, mimea, mazao ya kilimo na mifugo imesombwa na maji yavumayo kwa kasi.
Akitoa takwimu za watu waliokufa maji na kuathirika, waziri Wamalwa pia amesema kufikia wiki ijayo serikali itatoa taarifa kamili kuhusu kiwango cha mashamba, mimea na mazao yaliyosombwa na maji.
Kulingana na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, kiwango cha mvua kinaendelea kupungua.
Waziri hata hivyo ametahadharisha kwamba maeneo ya Magharibi mwa Kenya na Nyanza yataendelea kupokea mvua hadi Juni 2020.
Jumla ya kaunti 33 zimetajwa kuathirika na mafuriko yaliyoshuhudiwa mwezi Aprili na Mei.
“Tunahakikishia waathiriwa serikali itaendelea kuwapa chakula cha msaada,” waziri akasema.
Wamalwa pia amehimiza serikali za kaunti zishirikiane kikamilifu na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa.
Akipongeza idara hiyo, waziri amesema taarifa za mara kwa mara inazotoa zimesaidia serikali katika upangaji wa mikakati ya kuangazia athari za mafuriko.