Habari

Magari aina ya Renault Trucks yaanza kuundiwa kiwandani KVM Thika

October 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

MAGARI mapya aina ya Renault Trucks yameanza kuundwa rasmi katika kiwanda cha magari cha KVM mjini Thika.

Hafla hiyo iliyozinduliwa Ijumaa, Oktoba 25, 2019, mjini Thika, ilifunguliwa rasmi na katibu wa viwanda, mauzo, na ushirika, Dkt Francis Owino kwa niaba ya waziri Peter Munya. Ilishuhudiwa na Rais wa kampuni ya Renault Trucks, Bruno Blin, na mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina.

Blin alipongeza juhudi ya Kenya kuwapa nafasi ya kuwekeza nchini.

Alisema ushirikiano huo wa kuwekeza hapa nchini utazidi kuendelezwa hadi eneo pana la Afrika Mashariki kwa minajili ya kupiga hatua zaidi kibiashara.

“Tunafurahia kuwa hapa nchini huku tukitoa hakikisho kuunda magari bora aina ya Renault Trucks, na tunatarajia kuajiri wafanyakazi wapatao 200 kwa mkupuo mmoja. Hii inatokana na juhudi zetu za kufika hapa ili kuwekeza,” alisema Blin.

Alisema tayari wamefungua kituo cha mafunzo cha Al Fataim Academy eneo la Kusini mwa kanda ya Afrika Mashariki kitakachofunza ujuzi wa kuunda magari hayo.

Alisema tayari wamefungua matawi mengine ya kuunda magari ya Renault barani Afrika katika nchi za Tunisia, Algeria, Ivory Coast, Senegal, na Guinea.

Katibu Dkt Owino naye alisema kuwekeza kwa kampuni hiyo ya Renault Truck kunatilia mkazo ajenda nne muhimu za serikali ambapo mojawapo ni ujenzi wa viwanda ili kuleta ajira.

Uimarishaji wa uchumi

Alisema jinsi wawekezaji wanavyofika hapa nchini ndivyo wanaendelea kuimarisha uchumi wetu.

Alisema Kenya inatarajia kuinua uchumi wake wa GDP kutoka asiliia 7.7 hadi asilimia 15 ifikapo 2022 huku akiongeza kuwa uwajibikaji utafanikisha mipango hiyo.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle Wainaina alipongeza juhudi za serikali kualika wawekezaji kutoka nchi za nje ili kuwekeza hapa nchini.

Alisema nchi ya Kenya inastahili kuiga taifa la China ambalo linaendesha biashara zake chini ya taratibu za kiuchumi za muda wa saa 24.

“Tunajivunia kuwa na barabara kuu ya Thika Superhighway ambayo itakuwa muhimu kwa usafirishaji wa vipuri muhimu kutoka Nairobi vikiletwa hapa mjini Thika,” alisema Bw Wainaina.

Alieleza kuwa kwa muda mrefu mji wa Thika ulikuwa umebahatika kuwa na viwanda vingi ambapo umetajwa kama mmojawapo wa miji safi hapa nchini kwa kuhifadhi mazingira.

Alisema mji wa Thika pia inajivunia kuwa na viwanda vingi na hiyo ni njia moja ya kukuza uchumi wa Kenya huku ikitoa ajira kwa vijana wetu.

“Iwapo tutashikilia msimamo huo, mji wa Thika utaangaziwa katika ramani ya ulimwengu kutokana na kuinua uchumi wa nchi,” alisema mbunge huyo.