Magavana sasa wataka kikao cha dharura na Rais
Na BENSON AMADALA
BARAZA la Magavana (CoG) linamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuandaa kikao cha dharura ili kutafuta suluhisho la mzozo wa ugavi wa mapato ambao umelemaza shughuli katika kaunti.
Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, ambaye ndiye mwenyekiti wa CoG, alisema mvutano uliopo kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato 2019, umetumbukiza serikali za kaunti katika matatizo ya kifedha na kulemaza utoaji huduma muhimu kwa wakazi.
“Kwa sasa, pesa pekee tunazoweza kufikia ni zile za Wizara ya Fedha zilizosongezwa mbele kutoka mwaka uliopita wa fedha, na mapato yanayokusanywa katika kaunti. Kaunti zinakumbana na hali ngumu sana kwa sababu ya mivutano ya ubabe kati ya Bunge na Seneti,” alieleza Bw Oparanya.
Kulingana na Bw Oparanya, magavana wako tayari kufanya kikao na Rais Kenyatta kupata maafikiano ili fedha zitolewe kwa kaunti pasipo kupoteza muda zaidi.
“Wakati umewadia kwa Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati mzozo huu na kuitisha kikao cha magavana ili tuafikiane mgawo wa fedha utakaotolewa kwa serikali za kaunti. Hali inazidi kudorora siku baada ya nyingine,” akasema Gavana huyo wa Kakamega.
Bw Oparanya alikuwa akizungumza jana katika makao makuu ya kaunti hiyo. Alisema mvutano huo wa ugavi wa mapato, ambao umedumu kwa miezi miwili, umewaletea maafa wakazi kwani umelemaza huduma muhimu na kusababisha matatizo chungu nzima ikiwemo uhaba wa dawa za matibabu katika vituo vya afya.
Alihimiza magavana wenzake kubuni mbinu za kuimarisha ukusanyaji mapato ya kaunti ili kuondoa tegemeo la fedha za mgawo.
“Nguzo yetu ni katika ukusanyaji wa mapato yetu wenyewe. Tunachohitaji kufanya ni kuweka mbinu mwafaka za ukusanyaji ili tuzidishe kiwango cha mapato ya kaunti. La sivyo, huduma muhimu kama za matibabu na katika sekta zingine muhimu zitalemezwa kwa muda mrefu sana,” akaeleza.
Mwezi jana, Bw Oparanya aliwatuma nyumbani kwa likizo ya lazima maafisa 143 katika ofisi ya ukusanyaji mapato na kutangaza mikakati ya kuimarisha shughuli hiyo katika masoko na maeneo mengine ikiwemo Hospitali Kuu na Rufaa ya Kaunti.
Ukusanyaji mapato
Vilevile, aliagiza mawaziri na maafisa wakuu wa idara kusimamia na kuendesha ukusanyaji mapato katika kaunti zote ndogo 12 za Kakamega kwa miezi miwili ijayo.
Tangu kufanya mabadiliko hayo, alieleza Bw Oparanya, mapato yaliyokusanywa katika kaunti hiyo ya Kakamega yameongezeka mara nne.
“Niko na uhakika tunaweza kukusanya hadi Sh2 bilioni, tukiendelea na mkondo ambao umeshuhudiwa katika majuma mawili yaliyopita. Ni dhahiri kwamba tumekuwa tukipoteza mamilioni ya pesa kwa sababu ya mbinu duni na mianya katika mifumo ya ukusanyaji, ambayo imesababisha kutoweka kwa mapato,” akasema ofisini mwake.