Magavana wakumbatia Mpango wa Afya Kwa Wote
Na WINNIE ATIENO
MAGAVANA wamekubali kutekeleza Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukubali mapendekezo yao.
Mnamo Ijumaa, Baraza la Magavana lilisisitiza msimamo wake wa kupinga utekelezaji wa UHC, likisema hakukuwa na ufadhili wa kutosha.
Baraza hilo lilidai kuwa majaribio ya mpango huo katika kaunti za Machakos, Isiolo, Nyeri na Kisumu, yalikabiliwa na changamoto nyingi.
Walisema wakati wa majaribio katika kaunti tano, ulikubwa na ukosefu wa pesa na mipango duni ya utekelezaji kwa kukosa sera ya kuufanikisha.
Hata hivyo, mnamo Jumamosi, viongozi hao wa kaunti wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza hilo Bw Wycliffe Oparanya walilegeza masimamo wao na kuukubali baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukubali mapendekezo waliyotoa kuufanya ufanikiwe.
Walisema kwamba watauunga kwa asilimia 100 iwapo matakwa yao yatazingatiwa.
Miongoni mwa matakwa hayo ni kubuniwa kwa hazina ya UHC, kuajiriwa kwa wafanyakazi wa UHC, kufanyia mageuzi Bima ya Afya Nchini (NHIF) ikiwemo kufanyia marekebisho sheria kuhusu NHIF ili kuruhusu uwakilishaji wa kaunti katika bodi ya shirika hilo.
Katika taarifa ya pamoja iliyotiwa sahihi na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, mwenzake wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na CoG, masuala tisa yaliafikiwa ili kufanikisha UHC.
Walikubaliana kuhusu kubuniwa kwa hazina ya UHC inayojumuisha kaunti kuhusu bima ya afya katika jamii ambayo mipango yake inaendelezwa, kukamilisha sera ya UHC kwa kushauriana na wadau zikiwemo kaunti, kupata mfumo wa bima unaohakikishia ufadhili wa huduma ya afya ya kimsingi, kujikinga na kujiimarisha kiafya ili kufanikisha mpango huo.
Wizara ya afya, ilisema itahamisha mishahara ya madaktari kwa kaunti pindi Bodi za Huduma za Kaunti zitakapokamilisha michakato ya ajira na kuwasilisha mapato kufikia Januari 1.
Siku zijazo ni bodi husika za kaunti zitakazoajiri wafanyakazi.
Wizara itatoa raslimali panapohitajika kwa mafunzo ya maafisa wa afya wa kujitolea na malipo kwa kaunti husika.
Wizara hiyo pia ilikubali kutoa ufadhili kwa kaunti kununua vifaa kwa vituo vya afya vya Level 3 na Level 2.
UHC itawezesha Wakenya kupata huduma kadhaa muhimu za afya ikiwemo huduma kwa wagonjwa wasiolazwa na waliolazwa, usimamizi wa maradhi ya kuambukizwa na yasioambukizwa, huduma za uzazi, matibabu ya figo, saratani, afya ya kimawazo, upasuaji mdogo na mkubwa, urekebishaji kutokana na matumizi ya mihadarati, huduma za dharura miongoni mwa mengine kwa kiasi cha chini cha Sh6,000 kwa kila familia kila mwaka.