HabariSiasa

Magavana walia kuteswa na maseneta

May 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

MAGAVANA wamelalamika kuwa maseneta wanawapiga vita wakitumia vikao vya kuwahoji kuhusu matumizi ya pesa za umma.

Viongozi hao wa kaunti wameonyesha kuchukulia zoezi hilo, ambalo linaelekea kukamilika, kama mapambano ya kisiasa na maseneta wa kaunti zao.

Maseneta wamekuwa wakiomba kuketi kwenye vikao wakati magavana wa kaunti zao wanapohojiwa.

Baadhi ya magavana ambao wamekabiliana na maseneta wa kaunti zao katika vikao vya mbeleni ni Okoth Obado na Ochilo Ayacko wa Migori, Mohammed Kuti na Fatuma Dulo (Isiolo), Ferdinand Waititu na Kimani Wamatangi (Kiambu), Mike Sonko na Johnson Sakaja (Nairobi), Kiraitu Murungi na Mithika Linturi (Meru), Josephat Nanok na Prof Malik Ekai (Turkana).

Wakati wa zamu ya Bw Obado, gavana huyo alifika mbele ya kamati tayari kwa makabiliano, akisema kuwa endapo Seneta Ayacko angemshambulia angemjibu papo hapo.

“Bw Mwenyekiti ikiwa seneta wangu atanirarua, pia nami nipewe fursa ya kumrarua,” Bw Obado akasema alipopewa fursa ya kusema kabla ya kikao kuanza.

Hali ilikuwa sawa wakati zamu ya Gavana Waititu wa Kiambu ilipofika, ambapo Seneta Wamatangi akimkaanga kuhusu bajeti iliyokuwa na utata, nacho kikao hicho kikitawaliwa na majibizano. Seneta Wamatangi alisukuma kamati hadi ikaamrisha Mkaguzi Mkuu afanyie kaunti hiyo ukaguzi tena, japo Bw Waititu alidai vilikuwa vita vya kisiasa. Baadaye, alihutubia wanahabari na akamlaumu Bw Wamatangi kuwa alipeleka siasa za kaunti katika kamati.

“Nilishangaa kufika pale, na seneta ambaye ndiye anafaa kutetea kaunti yetu alikuwa wa kwanza kutuaibisha,” akasema Bw Waititu.

Bw Linturi na Bw Murungi nao walishambuliana katika kikao wakati wa zamu ya Kaunti ya Meru. Hali sawa ilishuhudiwa wakati wa zamu ya Bw Kuti.

“Bw Mwenyekiti nahisi vibaya sana wakati nina mradi mzuri wa kuinua maisha ya akina mama wetu, lakini seneta anataka kuupiga siasa kuumaliza. Hizi ni siasa tupu,” Gavana Kuti akasema alipokuwa mbele ya kamati wiki iliyopita.

Magavana wa Kirinyaga, Pokot Magharibi, Kilifi, Mombasa, Homa Bay na Murang’a pia wanatarajiwa kufika mbele ya kamati hiyo.

Hisia sawa jana ziliibuliwa na makundi ya uanaharakati, yakimtaka mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Uhasibu, Moses Kajwanga kuchukua hatua, kuhakikisha vita vya kisiasa havitumiwi na wanachama wa kamati hiyo kuwahangaisha magavana.