Habari

Mahabusu ajitoa uhai seli baada ya kushindwa kumshawishi mamake afute kesi

Na TITUS OMINDE February 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHABUSU mwenye umri wa miaka 24 anayekabiliwa na shtaka la kuvunja baa ya mamake na kuiba pombe alijiua katika seli ya Mahakama ya Eldoret Jumatano, baada ya jaribio lake la kumshawishi mamake aondoe kesi hiyo kuonekana kugonga mwamba.

Collins Cheruiyot anadaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya long’i yake mara baada ya kupiga simu kumshawishi mamake kufika kortini ili kusuluhisha suala hilo bila mafanikio.

“Kabla ya kujitoa uhai katika seli ambayo haikuwa ikitumika alikuwa amempigia simu mamake akimsihi afike kortini kuondoa kesi hiyo na kumsamehe,” alisema mmoja wa wafungwa katika seli hiyo.

Cheruiyot ambaye aliomba kwa mara ya kwanza Mei 27, 2024, alikiri hatia kwanza kabla ya kubadilisha ombi lake la kuwa hana hatia.

Tangu wakati huo kesi yake imekuwa ikiahirishwa mara kadhaa huku akiiomba mahakama kumsubiri mamake aondoe kesi hiyo.

Mnamo Jumatano alifika mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Kimani Mukabi ambaye aliagiza kesi hiyo itajwe Machi 27 kwa maelekezo zaidi.

Hati ya mashtaka ilisema kuwa mnamo Mei 24, 2024 katika Kituo cha Biashara cha Burnt Forest katika Kaunti Ndogo ya Ainabkoi alivunja na kuingia katika Baa ya Round Point kwa nia ya kuiba kutoka kwa baa hiyo.

Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Turbo Patrick Wekesa alisema juhudi za polisi na wahudumu wa mahakama na wafungwa wengine kumwokoa hazikufua dafu kwani alitangazwa kuwa amefariki alipofika katika Hospitali ya MTRH ambako alikimbizwa kwa matibabu.

Polisi wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.