Mahakama yaamuru serikali iwasilishe ripoti kuhusu virusi vya Corona
Na RICHARD MUNGUTI
SERIKALI Ijumaa imeagizwa na Mahakama Kuu iandae ripoti na kuiwasilisha kortini jinsi inavyojiandaa kukabili virusi vya Corona – Covid-19 – nchini.
Jaji James Makau aliamuru Wizara za Afya , Uchukuzi na Usalama kupitia kwa mwanasheria mkuu ziwasilishe ripoti jinsi imejisatiti na kujiandaa kukabili gonjwa la Cocid-19 endapo litazuka hapa nchini.
Jaji Makau pia aliamuru ripoti iwasilishwe kortini kuwahusu abiria 239 kutoka Uchina waliongia nchini Feburuari 26.
Jaji huyo aliamuru ripoti iwasilishwe ikiwa abiria hao 239 wamezuiliwa katika mojawapo ya Vituo vya Kijeshi nchini (KDF).
Mahakama ilielezwa ndege iliyowabeba raia hao wa Uchina iliingizwa kwa siri katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Jaji huyo alifahamishwa na wakili Henry Kurauka afya ya umma ni moja wapo wa haki zinazotangazwa katika Katiba.
“Afya ya kila Mkenya imepewa kipaumbele katika Katiba. Ni jukumu la Serikali ya kitaifa kuhakikisha kila Mkenya ana afya nzuri,” amesema wakili Kurauka.
Wakili huyo aliyewasilisha kesi kwa niaba ya Madaktari Josephine Mwenda na Cyprian Thiakunu amemweleza Jaji Makau kwamba “wananchi wenye afya ndiyo rasilimali kuu ya kila nchi.”
Wiki iliyopita kesi tatu ziliwasilishwa kortini huku walalamishi wakiomba watu kutoka nchi ambazo zilitambuliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) wasikubaliwe kuingia nchini Kenya.
Jaji Makau aliamuru Serikali, kupitia asasi zifaazo, isiwakubalie watu wa nchi zilizotangazwa na WHO kuingia nchini Kenya.
Pia jaji huyo ameamuru serikali iweke mikakati tosha ya kuwapima wageni wanaoingia nchini Kenya kubaini ikiwa wana Covid-19 au la kama njia ya kuzuia wasiwaambukize wananchi.
Kufikia sasa hakuna raia wa Kenya ameambukizwa virusi vya Corona ambavyo vimesababisha maelfu ya raia wa China kukata kamba.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema vipimo vya visa 31 vilivyoshukiwa vimebainisha hakuna maambukizi ya virusi vya Corona nchini.
Ameongeza kwamba idadi ya maafisa 1,100 wa afya tayari wamepewa mafunzo ili waweze kukabiliana na virusi hivyo iwapo kutatokea dharura ya aina hiyo.