Mahakama yazima uteuzi wa Wambui kusimamia uajiri
Na RICHARD MUNGUTI
UTEUZI wa aliyekuwa Mbunge wa Othaya Mary Wambui kuwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uajiri (NEA) na Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2019 umefutiliwa mbali na Mahakama ya Kuamua Mizozo ya Waajiri na Wafanyakazi (ELRC).
Akifuta uteuzi huo , Jaji Onesmus Makau, alisema Wambui hajahitimu kuongoza mamlaka hiyo.
“Uteuzi wa Bi Wambui ulikaidi vipengee vya Katiba na masharti yaliyowekwa,” alisema Jaji Makau.
Jaji huyo alifutilia mbali uteuzi uliotangazwa Oktoba 14, 2019, katika Gazeti rasmi la Serikali.
“Hii mahakama imetilia maanani ushahidi uliowasilishwa na walalamishi na imeridhika kabisa Bi Wambui hastahili kuteuliwa kutekeleza majukumu ya NEA,” alisema Jaji Makau.
Kuteuliwa kwa Bi Wambui kusimamia NEA kulizua hisia kali kutoka kwa umma na makundi ya kijamii wakisema mbunge huyo wa zamani “hana uhusiano wa karibu na vijana wengi waliohitimu vyuo vikuu nchini na wanaotafuta ajira.”
Walalamishi pia walihoji uwezo wa mwanasiasa huyo kumudu NEA.
Seneta maalum Bi Millicent Omanga wa chama kinachotawala cha Jubilee alisema uteuzi huo wa Bi Wambui na Rais Kenyatta ulidhihaki vijana wa nchi hii waliohitimu katika taaluma mbalimbali.
Punde tu baada ya uteuzi huo Jaji Hellen Wasilwa alitoa agizo la kumzuia Bi Wambui akitwaa hatamu za afisi hiyo ya NEA kufuatia kesi iliyoshtakiwa na Chama cha Wabunge Vijana (KYPA) ambacho mwenyekiti wake ni Seneta wa Nairobi Bw Johnson Sakaja.
KYPA kilisema Bi Wambui hajahitimu kwa mujibu wa katiba na sheria kuongoza NEA.
Walalamishi walidokeza mara kadha, mbunge huyo wa zamani alikiri hajahitimu kielimu na hivyo ikawa ni vigumu kwake kuongoza NEA.
KYPA alisema Bi Wambui hakutimiza masharti ya Kifungu nambari 10 (2)(c) cha sheria za uajiri za NEA.
Masharti yaliyotangazwa ya uteuzi wa mwenyekiti ni makali na lazima yafuatwe.