Mahakama yakataa kufuta baadhi ya vifungu vinavyopinga ushoga na usagaji
Na RICHARD MUNGUTI
WANAOENDELEZA ushoga na usagaji nchini Kenya wameondoka katika mahakama kuu wakiwa wamesononeka baada ya tabia hiyo kuharamishwa.
Majaji watatu walitupilia mbali kesi yao na kusema “hawana nafasi nchini.”
Mashoga na wasagaji waliokuwa wamejipodoa walimiminika katika Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi wakiwa na matumaini kwamba wataruhusiwa kushiriki ushoga na usagaji lakini majaji watatu wa mahakama kuu waliharamisha vitendo vyao.
Majaji hao; Roselyn Aburili, Enoch Chacha Mwita na John Mativo walisema ushoga na usagaji hauruhusiwi katika sheria za Kenya.
Majaji hao walisema sheria za humu nchini hutambua tu uhusiano baina ya mwanamume na mwanamke.
Sheria za humu nchini hutetea haki kati ya jinsia hizi tofauti na wala sio jinsia moja.
Majaji Aburili, Mwita na Mativo walitupilia mbali ombi la kundi linalopigania kutambuliwa kwa haki za wanaoendeleza ushoga na usagaji.
Kubaguliwa
Kundi hili lilitaka mahakama itangaze kwamba wanaoshiriki katika uhusiano wa jinsia moja wanabaguliwa.
Kundi la kitaifa la mashoga na wasagaji chini ya mwavuli wa LGBT lilikuwa limeomba mahakama ifutilie mbali sheria inayopiga marufuku ushoga na usagaji.
LGBT walisema haki za wanaoshiriki ushoga na usagaji zimekandamizwa na sheria.
Kifungu cha sheria kilichotakiwa kifutiliwe mbali ni Nambari 162 (a) na (c) cha Penal Code.
Kifungu hiki cha sheria kinapiga marufuku ushoga na usagaji.
LGBT walisema kifungu hiki kinakinzana na Kifungu 27 cha Katiba kinachosema kila mmoja anahitaji kutetewa na sheria.
LGBT walidai haki za wateja wao zinakandamizwa.
“Sheria haiwabagui wasagaji na mashoga kwa vile Katiba inatambua uhusiano usiokinzana na kKatiba na sheria zinazochangia maadili mema,” walisema majaji hao watatu.
Kifungu hiki nambari 162 (a) na (c) za Sheria za Kenya kimesema bayana wanaoendeleza uhusiano wa jinsia moja wanavunja sheria.
Sheria hii inasema: “Yeyote anayehusiana kimapenzi na mwiningine wa jinsia moja amevunja sheria na anastahili kufungwa jela miaka 14 gerezani.”
Majaji hao watatu walitumia kifungu hiki kutupilia mbali kesi hii ya LGBT.
“Tumetilia maanani mawasilishi yote ya walalamishi na mwanasheria mkuu na kufikia uamuzi kwamba Kifungu nambari 162 za Sheria za Kenya haikinzani kamwe na Katiba ya Kenya iliyopitishwa mwaka 2010,” wakasema majaji hao.
Waliongeza kusema, “Sheria iwazi kwamba ushoga na usagaji haukubaliwi nchini Kenya.”
Majaji hao walikataa mawasilisho ya watetezi wa ushoga kwamba tabia hiyo isiharamishwe kwani itakuwa sawa na kuwabagua.