Habari

Makabiliano eneo la Mikululo yasababisha vifo vya watu wawili

July 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

WATU wawili wameuawa na wengine sita wakajeruhiwa Jumamosi kufuatia makabiliano mapya baina ya wafugaji kutoka kaunti za Kajiado na Makueni katika shamba kubwa la ekari 42,000 lililoko eneo la Mikululo.

Shamba hilo ambalo umiliki wake umezua joto kali lipo kati ya kaunti ya Makueni na Kajiado.

Walioshuhudia shambulio hilo wameambia Taifa Leo kwamba kundi moja lilivamia lingine alfajiri.

Kulingana na mwenyekiti wa shamba hilo Bw Wilson Ndulu, kundi moja lilivamia lingine alfajiri na kuteketeza nyumba zao huku wafugaji kadhaa wakijeruhiwa na wengine kuuawa.

“Shambulio limetekelezwa mwendo wa saa 10 alfajiri Jumamosi,” Kamishna wa kaunti ya Makueni Mohammed Maalim amewaeleza wanahabari.

Bw Maalim hata hivyo amekataa kusema mengi kuhusu makabiliano hayo akisema tu “ni suala nyeti.”

Kamishna huyo amesema maafisa wa usalama kutoka kaunti ndogo za Makindu na Mashuru wamepelekwa mahala hapo pa tukio hilo kudumisha Amani.

Waliohjeruhiwa wamepelekwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Makindu kupokea matibabu.

Hili sio shambulio la kwanza kutokea katika eneo hilo kwa vile kumekuwa na kesi kuhusu umiliki wa shamba la Mikululo kati ya wakazi wa kaunti ya Makueni na Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS).

Mfugaji mmoja aliuawa mwaka 2019 katika mazingira sawa na ya tukio la Jumamosi.

Miaka michache iliyopita maafisa wa KWS walikuwa wanateketeza nyumba za watu katika juhudi za kutaka wahame.

Mwaka 2019 Mahakama Kuu Machakos ilitoa umauzi mnamo Februari 2019 kuhusu umiliki wa shamba hilo.

Jaji Oscar Angote, aliyeamua kesi hiyo baada ya kusikizwa kwa muda wa miaka 24 alisema shamba hilo linamilikiwa na wakazi wa Makueni.

Jaji Angote alisema KWS imekuwa ikijaribu kunyakua shamba hilo na kuikemea huku akisema “hatua hiyo inakiuka Katiba.”

Jaji huyo ailing’atua KWS kutoka shamba hilo na kuamuru isithubutu kuwatimua wakazi hao kutoka shambani humo.

Hatua hii ya kuwapa wakazi wa Makueni shamba hilo iliwaudhi wafugaji kutoka Kaunti ya Kajiado.

Wafugaji hao kutoka Kaunti ya Kajiado wanaona uamuzi huo kama kizingiti cha kuwazuia wasilishe mifugo wao kwenye shamba hilo.

Bw Maalim na mwenzake kutoka Kajiado Bw Joshua Nkanatha, wametoa wito kwa makundi hayo ya wafugaji waishi kwa amani.