Makanisa na wahubiri walalamikia kasi ya kupitisha Mswada wa kudhibiti makanisa
CHAMA cha Makanisa na Wahubiri Nchini (CCAK) kimepinga vikali kile kinachotaja kuwa mpango wenye upendeleo wa serikali kuharakisha kupitishwa kwa Sera ya Mashirika ya Kidini 2024 na Mswada wa Mashirika ya Kidini 2024.
Kupitia kwa mwenyekiti wake wa kitaifa, Askofu Hudson Deda, chama hicho kilieleza kusikitishwa na hatua ya serikali kutojumuisha maoni ya viongozi wa makanisa ambayo yaliwasilishwa kuingizwa katika rasimu ya mwisho kabla ya kupelekwa kwa ushirikishaji wa umma.
Katika taarifa ya Desemba 12, chama hicho kilisema kilishtushwa na notisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, iliyoitisha ushirikishaji wa umma kuhusu mswada huo unaolenga kuongoza shughuli za taasisi za kidini nchini.
“Tunatambua kuwa ushirikishaji wa umma umejengwa ndani ya Katiba, na kwamba Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri inajaribu kutekeleza wajibu huo. Hata hivyo, makanisa na wahubiri nchini wana wasiwasi kuhusu muda na kasi kinachotumika kuendesha mchakato huu,” alisema Askofu Deda.
Aidha, chama hicho kilisema kuwa ingawa kikao cha mwisho cha kamati ya pamoja, kilichohudhuriwa na Bw Mudavadi, kilikubaliana kufanyika kwa mkutano mwingine na Mwanasheria Mkuu, kikao hicho hakijafanyika jambo linaloibua maswali kuhusu nia ya serikali.
Pia chama hicho kilisema kuwa juhudi zake za kumfikia Katibu wa Wizara ya Uratibu wa Kitaifa, Ahmed Abdisalan Ibrahim, hazijafaulu.
“Kwa mshangao wetu, tuliona tena ule mwaliko wa awali wa ushirikishaji wa umma ambao tulipinga. Tuliwasiliana na Mheshimiwa Ahmed, akatuahidi kuwa baada ya kupokea maoni, tutafanya mkutano mwingine pamoja. Kwa bahati mbaya, tumeachwa nje, na sasa tunashuhudia mwito mwingine wa ushirikishaji wa umma kuhusu hati ambayo sisi hatuijui,” alisema Askofu Deda.
Kwa mujibu wa notisi ya serikali, wananchi wametakiwa kuwasilisha maoni yao kuhusu mswada huo kati ya Desemba 10 na 15, 2025.
Mswada huo uliandaliwa na jopo kazi lililoongozwa na Padre Mutava Musyimi, lililoanzishwa kufuatia vifo vya waumini wa dhehebu la Shakahola ambapo kufikia sasa zaidi ya miili 400 imefukuliwa, mojawapo ya maafa mabaya zaidi ya imani potofu nchini.
Ingawa lengo la mswada ni kudhibiti shughuli za taasisi za kidini na kuzuia maafa kama ya Shakahola, makanisa, yaliyotajwa kuwa wadau wakuu, yanataka uwazi na muda wa kutosha kushughulikia mapungufu yanayodaiwa kupatikana.
“Tunasoma hila katika muda uliotolewa, kwani Disemba ni mwezi ambao wahubiri wengi wana majukumu mengi. Muda uliotolewa hautoshi kutupatia nafasi ya kushughulikia sera na mswada huu ipasavyo, tunavyoona, serikali imelenga kuhakikisha mswada unapitishwa haraka. Hii ni kinyume cha Katiba,” chama hicho kilisema.
Aidha, Askofu Deda alisema kuwa mara tu nyaraka hizo zitakapopitia hatua ya ushirikishaji wa umma, haitakuwa rahisi kwa maoni ya viongozi wa dini kuingizwa mwishoni mwa mchakato wa utungaji sheria.
“Kanisa na wahubiri nchini wanapinga hatua hii ya ushirikishaji wa umma. Mchakato huu hauna baraka zetu,” alisema Askofu Deda.