Habari

Makanisa yakataa 'siasa' katika maabadi

April 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

MAKANISA makuu nchini yamewaagiza viongozi wake wasiruhusu wanasiasa kupiga siasa au kuongoza harambee za kuchangisha pesa katika makanisa yao.

Kanisa Katoliki na lile la Anglikana yanasema kuruhusu wanasiasa kufanya hivyo ni kuchafua jina la nyumba za ibada.

Ingawa hawakutaja wanasiasa kwa majina, huenda wakuu wa makanisa hayo mawili wamechukua uamuzi huo kutokana na mtindo wa wanasiasa maarufu kualikwa na kuchanga mamilioni ya pesa kanisani, hali ambayo imesababisha makanisa kukashifiwa kuwa yanaangazia pesa kuliko kuabudu Mungu.

Kanisa Katoliki lilianza hatua hiyo Alhamisi, wakati Muungano wa maaskofu wake (KCCB) ulitangaza kuwa umepiga marufuku wanasiasa katika makanisa yake, ukisema wanaingiza siasa kanisani na ‘kuchafua’ waumini.

“Majuzi, tulikuwa na mkutano wa maaskofu ambapo tulipitisha kauli kuwa hatutaruhusu wanasiasa kuingilia masuala ya kanisa na waumini, ama kuleta siasa katika makanisa yetu,” akasema Askofu David Kamau anayesimamia eneo la Nairobi.

Ijumaa, kanisa la Anglikana nalo lilifuata mkondo huo, Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit akisema kanisa hilo limeharamisha ualikaji wa wanasiasa na kuwapa fursa za kuhutubia waumini kama wageni wa heshima, huku wakijigamba.

Bw Sapit aliamrisha viongozi wa kanisa hilo wakome kuwapa wanasiasa majukwaa kanisani kwa kuwa wanachafua nyumba za ibada, na kusema yeyote anayetaka kuhusika katika michango afanye hivyo kwa upole kama waumini wengine, wala si kwa majigambo.

Alijutia kuwa ufisadi umeingizwa hadi kwenye makanisa nchini, akidokeza kanisa la Anglikana linawazia kukomesha kabisa michango ya harambee.

“Inahuzunisha kuwa ufisadi umekita mizizi katika kanisa na maisha ya wale wanaofuata imani za Biblia. Sisi katika makanisa sharti tuwajibike kuhusu ubaya huu na matendo yetu.”

“Ingawa tunafahamu umuhimu mkubwa ambao harambee zimekuwa nao katika maendeleo ya jamii, kanisa la Anglikana linawaza pia kuhusu uandaaji wa hafla hizo katika makanisa yetu na wanasiasa na watu tunaowataja wageni wa heshima. Wakristo, wakiwamo wanasiasa wanatarajiwa kumwabudu Mungu na kutoa mchango na sadaka kimya kama Biblia inavyofunza,” Bw Sapit akasema.

Maadili yako wapi?

Askofu huyo Mkuu aidha alisema japo Kenya imekuwa na sifa nzuri kimaadili na kidini, miaka ya majuzi maadili yamepotea na hata makanisa kuathirika, hali ambayo alisema kanisa halijafurahia.

“Umuhimu wa maadili na bidii ya kufanya kazi umepotea kadri miaka inavyosonga katika makanisa yetu, serikali na sekta ya umma. Hili ni kutokana na tamaa kubwa,” akasema Bw Sapit.

Hatua ya makanisa hayo mawili inafuatia ile ya viongozi wa kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) ambalo liliamua kuharamisha michango kama hiyo siku ya Sabato baada ya mgawanyiko mkubwa kutokea kuhusu hafla ya kuchangisha fedha iliyofanyika mjini Kisii.

Ujumbe wa makanisa hayo wakati makanisa yamekuwa yakikashifiwa, kutokana na hali yake kualika wanasiasa na kuwaruhusu kutumia matamshi ya chuki kushambuliana, kanisani.

Makanisa aidha yamekuwa yakikosolewa kuwa yameweka pesa ambazo yanaletewa mbele, bila kujali zinakotoka, yakikashifiwa yanachangia katika donda la ufisadi, ambao unalemaza taifa.