Malkia aliyedunga mchumba kisu mara 25 kunyongwa
Na RICHARD MUNGUTI
MALKIA wa urembo katika Gereza la Lang’ata jijini Nairobi mnamo 2016, Ruth Kamande, Alhamisi alihukumiwa kunyongwa kwa kumuua mpenziwe kwa kumdunga kisu mara 25.
Punde tu baada ya Jaji Jessie Leesit kupitisha hukumu, familia ya marehemu Farid Mohammed, ambaye alikuwa yatima, iliambia Taifa Leo kuwa imefurahishwa na adhabu hiyo licha ya kuwa itachukua muda mrefu kuponya nyoyo zao.
Jaji Leesit alisema adhabu ya kifo aliyopitisha dhidi ya Bi Kamande itakuwa ni funzo kwa vijana, wasichana kwa wavulana, wanaopandwa na hasira, na badala ya kujiendea zao wanaua bila kujali, kufikiria na bila huruma.
“Mshtakiwa alimuua Farid Mohammed, aliyekuwa wa miaka 24, kwa kumdunga kisu mara 25. Hakuwa na sababu ya kumtoa uhai ila alikuwa na wivu kupindukia. Alikuwa amekusudia kumwangamiza Farid. Alikuwa mchoyo, mwenye wivu mwingi na mwenye roho ngumu.”
“Mshtakiwa alimdunga mpenziwe kisu mara 25 kana kwamba alikuwa anafurahia na kujiburudisha,” Jaji Leesit alisema katika uamuzi aliousoma kwa muda wa dakika 15 na sekunde 11.
Alisema kuwa mshtakiwa hakusikia miito ya majirani waliofika kumwokoa marehemu baada ya kupiga kamsa.
Jaji huyo alisema mshtakiwa ambaye sasa yuko na miaka 24, alikuwa amekusudia kumuua Farid kwa vile alimdunga mara nyingi kwa lengo la kumfanya aone uchungu mwingi na hatimaye kumuua.
Alisema kabla ya kitendo hicho, mshtakiwa alikuwa amemfungia marehemu ndani ya nyumba na kumzuia kwenda kazini kusudi asipatane na vidosho wengine na kuwachumbia.
“Mshtakiwa alikuwa na mazoea ya kukagua simu ya mpenziwe kwa lengo la kuchunguza ikiwa alikuwa anawasiliana na wasichana wengine. Marehemu alikuwa anakadamizwa na kutawaliwa na mshtakiwa,” akasema jaji.
Mahakama ilisema hata baada ya mshtakiwa kupewa fursa aeleze kilichosababisha amuue Farid, hakuweza kusema na kupelekea jaji kusema alikuwa amepanga kumuua.
Jaji Leesit alisema vijana wanaoua pasipo na sababu sasa watakuwa wanafikiria mara mbili kwa sababu adhabu ya kifo ingalipo licha ya mapendekezo ifutiliwe mbali.
“Licha ya kuwa nimechambua ushahidi wote na kusikiza malilio yako kuwa umejirekebisha na hata umepokea mafunzo ya kidini kutoka kwa kanisa la Presbyterian Church of East Africa (PCEA), ishara ya kuwa amebadilika, hukumu ni ile ile,” alisema Jaji Leesit.
Kuhusu suala la mshtakiwa kupata mwaliko wa kujiunga na chuo kikuu cha JKUAT, Jaji Lessit alisema Bi Kamande anaweza kupokea masomo hayo katika gereza, ambapo amekuwa akishiriki katika sanaa, densi na mashindano ya urembo.
Korti ilisema uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu adhabu ya kifo ulikuwa wa kutoa ushauri kwa majaji wanaosikiza kesi za mauaji
Mahakama ilimpa siku 14 kukata rufaa.