Habari

Mambo yaenda segemnege

August 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

HALI ya kuchanganyikiwa inayoshuhudiwa serikalini inatishia utoaji huduma, ustawi na udhabiti wa nchi iwapo mambo hayatalainishwa kulingana na Katiba, watathmini wa utawala na siasa wameonya.

Hii ni kufuatia hali ya kuchanganyikiwa ambapo viongozi wakuu wa serikali – Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto hawasikizani, vinara wa upinzani Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wamehepa majukumu yao na kujiunga na serikali huku Bunge la Kitaifa na Seneti zikifanya shughuli kwa uelekezi wa Serikali Kuu.

Idara ya Mahakama nayo imefifia kwa wakuu serikalini kupuuza maagizo yake, taasisi kuu za kupambana na ufisadi –Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) – wanavutana huku mashirika ya umma yakiingia mitini, nao wananchi wakibaki kulalamika baina yao na kwenye mitandao ya kijamii.

Ni hali hii ambayo wachambuzi wa siasa na utawala wanasema inatishia kulemaza utoaji huduma kabisa, kuendeleza ufisadi na kuyumbisha udhabiti wa nchi.

“Wakenya hawaelewi nchi yao inakoelekea wala pa kukimbilia wakiwa na shida, kwani taasisi za kikatiba zinazofaa kuwalinda zimekuwa mateka wa serikali. Nao viongozi wakuu serikalini kama vile Dkt Ruto wamechukua misimamo tofauti na majukumu yao yao ya kikatiba,” asema mbunge wa zamani aliyeomba tubane jina lake.

Dkt Ruto amegeuka mkosoaji wa serikali anayohudumia huku Bw Odinga na Bw Musyoka wakiunga mkono serikali wanayopaswa kukosoa.

Kulingana na mbunge huyo, serikali imekosa mpangilio wa kikatiba, ambao lengo lake ni kuwezesha ofisi na idara mbalimbali za serikali kufanya kazi kwa utaratibu ulionyooka.

“Kikatiba Dkt Ruto ni msaidizi rasmi wa Rais Kenyatta na hivyo hafai kumkosoa hadharani mkubwa wake. Viongozi wa upinzani nao wanafaa kukosoa serikali ili kuhakikisha inatawala kwa mujibu wa sheria na kutendea raia haki. Lakini sasa mambo ni tofauti na azma ya Katiba,” akasema.

Katika Bunge la Kitaifa na Seneti, washirika wa Dkt Ruto wametwaa majukumu ya upinzani huku wale wa vyama vya ODM na Wiper wakiungana na wanaomuunga mkono Rais Kenyatta katika upande mmoja.

WABUNGE VIBARAKA

Hali hii imefanya Bunge kushindwa kutekeleza majukumu yake makuu ikiwemo kupiga darubini utenda kazi wa serikali.

“Wabunge karibu wote wamekuwa vibaraka wa serikali. Wanatumiwa kama muhuri wa kuidhinisha sera na matakwa ya serikali bila kuyapiga darubini. Wanafuata maagizo ya viongozi wa vyama vyao kama kondoo ili wasiadhibiwe wakikaidi,” asema mtetezi wa haki za binadamu Ndung’u Wainaina.

“Mpangilio katika bunge unakanganya. Hauwezi ukatofautisha kati ya Kiongozi wa Wachache James Mbadi na Kiongozi wa Wengi Amos Kimunya. Wote wanatetea ajenda za serikali. Wale wanaomuunga Dkt Ruto ndio wamekuwa upinzani ilhali wanatoka chama cha Jubilee kilicho madarakani. Hii ni hali hatari kwa nchi,” asema mdadisi wa siasa Peter Ocheing ambaye pia ni wakili.

“Hali inayoshuhudiwa kwa sasa serikalini ni kuwepo kwa watu walio na ushawishi serikalini, ambao lengo lao kuu ni kupata utajiri. Hawana nia ya kuona mambo yakiendeshwa kwa mujibu wa sheria na haki, kwani hali ikinyooka watakosa nafasi ya kupora mali ya umma,” aeleza Bw Wainaina.

Idara ya Mahakama, ambayo kikatiba ina wajibu wa kuhakikisha kila Mkenya anatendewa haki, imegeuzwa gofu kwa wakuu kupuuza maagizo na maamuzi yake, kupunguziwa mgao wa bajeti pamoja na kukumbwa na uhaba wa majaji kutokana na hatua ya Rais Kenyatta kukataa kuapisha majaji 41 waliokuwa wameteuliwa na Tume ya Mahakama (JSC) mwaka 2019.

Kulingana na Jaji Mkuu David Maraga, hatua hiyo imesababisha kurundikana kwa kesi, wengi wa waathiriwa wakiwa raia wa kawaida.

“Uhaba wa majaji na kukwama kwa shughuli za korti umesababishwa na hatua ya Rais kukataa kuapisha majaji 41,” alisema Jaji Maraga mnamo Juni mwaka huu.

Wadadisi wanasema kwa kudharau mahakama na kuinyima pesa, serikali imefanya ufisadi kukita mizizi.

Sakata kubwa za ufisadi zinazohusisha watu wenye ushawishi serikalini zinaripotiwa katika kila sekta na washukiwa huchukuliwa hatua kwa kutegemea mwegemeo wao wa kisiasa.

Sakata ya hivi punde ya wizi wa pesa za kukabiliana na corona imechukua mkondo wa kisiasa baada ya viongozi wa Jubilee na washirika wao kutajwa.