Habari

Mamia wakwama Thika Road wakielekea Kasarani

Na WINNIE ONYANDO October 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

PINDI tu serikali ilipotangaza kuwa mwili wa Raila Odinga ungepelekwa katika Uwanja wa Moi Kasarani, mamia walifurika katika barabara ya Thika wakielekea uwanjani na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.

Umati mkubwa ulijitokeza kuusindikiza mwili wa Kiongozi huyo wa Upinzani kama ishara ya kutoa heshima zao za mwisho.

Hata kabla ya mwili wa Bw Odinga kufika katika uwanja huo, tayari watu walikuwa wamejaa huku mamia wakiendelea kufika katika eneo hilo.

Mwili wa Raila ulipokelewa kishujaa na waombolezaji ambao walisitisha shughuli katika uwanja wa ndege wa JKIA, baadhi wakifika karibu na ndege iliyobeba mwili wa Bw Odinga.

Licha ya usalama mkali, baadhi waliwazidi wanajeshi na kufikia jeneza ambalo lilikuwa limebeba mwili wa Tinga huku wakiomboleza kwa uchugu.

Umati huo uliwanyima nafasi Rais William Ruto, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, familia ya marehemu, viongozi wa serikali na wanasiasa kuupokea mwili kwa njia rasmi.

Wengi sasa wanasema kuwa serikali inafaa kuusafirisha mwili huo kutoka Kisumu kuenda Bondo kwa kutumia ndege kwani wengi watajitokeza Kisumu na maeneo karibu na kuzuia mwili kufika nyumbani kwa wakati.