Maporomoko: Watu 16 waendelea kutafutwa
SHUGHULI ya kuwasaka watu 16 ambao bado hawajapatikana baada ya maporomoko ya ardhi wikendi katika ukanda wa Bonde la Kerio imeingia siku ya sita.
Timu za uokoaji zilionya kuwa baadhi ya miili imezikwa kina cha fiti sita chini ya vifusi hivyo kutatiza juhudi za uokoaji.
Janga hilo liliacha familia zaidi ya 1,500 bila makao katika vijiji vinne eneo la Elgeyo Marakwet, ambapo waokoaji na wanajamii wanawasaka watu waliopotelea kwenye matope, miamba na kingo za mito.
Mamia ya wanakijiji wa Kipkirwon walikusanyika chini ya miembe Jumanne adhuhuri katika kanisa la Katoliki la St Benedict Christ the King Catholic, Chesengoch, kwenye mkutano uliopangwa na mamlaka eneo hilo kuwaarifu kuhusu maporomoko ya ardhi wikendi.
Kufikia Jumanne jioni, watu 34 walithibitishwa kufariki, 35 kujeruhiwa na 17 hawajulikani walipo.
Waziri wa Mazingira, Deborah Barasa aliyezuru maeneo yaliyoathirika, alisema familia zaidi ya 1,500 Elgeyo Marakwet zimefurushwa makwao na maporomoko hayo.
Wafanyakazi wa kutoa msaada hatimaye walifaulu kuwasilisha shehena za msaada Jumanne adhuhuri baada ya barabara muhimu, Sisiya-Kaspsiya, inayotoka Kapsowar kuelekea Chesongoch, kufunguliwa.Magari yalikwama kwa siku tatu kwa sababu ya barabara mbovu zisizopitika.
Janga hilo liliathiri familia nyingi eneo hilo, na huku timu za uokoaji zikiendelea na msako, simulizi za kuwapoteza wapendwa zimeshamiri kote katika vijiji jirani.
Familia zilizogubikwa na wasiwasi na majonzi zimejiunga na vikosi vya uokoaji kuchimba vifusi, kingo za mto, kuwasaka wapendwa wao waliotoweka.
Bi Susan Kaino, 45, mama wa watoto watano, ni miongoni mwa familia zinazoshikilia roho mikononi kwa matumaini ya kuwapata wapendwa wao.
Mwanawe Martin Kiptoo, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Egerton, ni mmoja kati ya watu 16 ambao bado hawajapatikana kufuatia janga lililosomba vijiji vya Kasegei, Kaptul, Kwenoi, na Kipkirwon, Ijumaa usiku.
“Tumetafuta maporomoko yote na mto, lakini Martin angali hajapatikana. Nataka kujua tu alipo na mahali pa kujenga upya maisha yetu,” alisema akizidiwa na simanzi.
Martin alirejea nyumbani kutokana na mgomo wa wahadhiri wa vyuo vikuu na alikaa nyumbani siku tatu tu kabla ya janga kuzuka.
Katika kijiji cha Kwenoi, Yano Cherop, 82, bado anasubiri habari kuhusu wajukuu wake watatu waliotoweka wenye umri kati ya miaka miwili na tisa.Jamaa wengine watatu wa familia wakiuguza majeraha mabaya katika Hospitali ya Rufaa ya Moi (MTRH), Eldoret.
Bw Emmanuel Kemboi, 42, vilevile kutoka Kwenoi, alimpoteza mama yake, dada yake anauguza majeraha MTRH, nyanya na wapwa wake watatu wangali hawajapatikana.