Maraga ahimiza Wakenya kuwafichua maafisa fisadi
Na WACHIRA MWANGI
JAJI Mkuu David Maraga amewaomba Wakenya watoe ushahidi dhidi ya majaji au mfanyakazi yeyote wa mahakama anayejihusisha na ufisadi.
Akihutubia waandamanaji waliojitokea Alhamisi jijini Mombasa, Bw Maraga alisema kuwa idara anayosimamia haina malaika na kuna uwezekano wapo wanaoendeleza ufisadi.
Hata hivyo, alisema kuwa ni ushahidi pekee utakaowezesha afisi yake kuwachukulia hatua wahusika.
“Ikiwa wenyeji wa Pwani wana suala lolote, Idara ya Mahakama iwazi kupokea malalamishi yao. Wanapaswa kuja kwangu. Siwezi kukataa kwamba idara hii ina visa vya ufisadi, sawa na asasi zingine,” akasema.
Waandamanaji hao walilamamika kuhusu kuongezeka kwa visa vya ufisadi miongoni mwa baadhi ya maafisa wa idara hiyo.
Walikita kambi katika hoteli ya Sarova Whitesands kulikokuwa na kikao maalum cha majaji kutoka kote nchini.
Wadai walanguzi watumia mahakama kujilinda
Waandamanaji walidai kwamba mahakama zimekuwa zikitumika na walanguzi wa mihadarati kujilinda dhidi ya kukabiliwa kisheria.
Walimtaka Rais Kenyatta kuwaondoa maafisa wote wa mahakama waliohusika kwenye kesi ya ndugu za Akasha, waliohukumiwa nchini Amerika wiki iliyopita kwa ulanguzi wa mihadarati.