Maraga: Upungufu wa majaji umeathiri pakubwa utendakazi wa idara ya mahakama
Na SAMMY WAWERU
HUKU Jaji Mkuu (CJ) David Maraga akijiandaa kustaafu rasmi Januari 2021 ameendelea kulalamikia uhaba wa majaji katika idara ya mahakama.
Bw Maraga amesema Ijumaa kwenye hotuba yake ya mwisho akijiandaa kufunganya virago kuondoka afisini, kwamba upungufu wa majaji umeathirika huduma za mahakama na utoaji wa haki kwa umma.
Akitumia mfano wa Mahakama ya Rufaa, amesema inahitaji zaidi ya majaji 30, ilhali kwa sasa ina majaji 16 pekee, takwimu inayoashiria inatekeleza majukumu yake na upungufu wa majaji 14.
“Hali hiyo pia inashuhudiwa katika mahakama zingine,” akasema CJ Maraga kwenye hotuba yake jijini Nairobi.
Alisema idadi ya kesi katika Mahakama ya Rufaa inaendelea kuongezeka, kutoka kesi 3,681 kipindi 2018/2019 hadi zaidi ya 4, 000 mwaka huu 2020.
“Idara ya mahakama inaendelea kulemewa na kazi kutokana na idadi ya juu ya kesi,” akasema.
Mwaka 2019 Rais Uhuru Kenyatta alikataa kuidhinisha uteuzi wa majaji 41 waliopendekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), kwa msingi kuwa baadhi yao walikuwa na dosari.
Hata hivyo, kulingana na Bw Maraga, licha ya walioteuliwa kutiliwa shaka, wanapaswa kuidhinishwa, akisema Katiba imeweka wazi mikakati kuwapiga msasa kupitia kamati ya muda itakayoundwa na JSC kuchunguza madai hayo.
“Ninaendelea kumhimiza Rais kuwaidhinisha bila kukawia,” CJ akasema.
Kwa sasa, kati ya majaji waliopendekezwa na JSC, wamesalia 40 baada ya mmoja wao kufariki.
Akifufua matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta ya baada ya ushindi wake 2017 kufutiliwa mbali na Mahakama ya Juu zaidi Nchini, “tutatathmini utendakazi wa Mahakama”, Bw Maraga amesema yameathiri kwa kiasi kikuu idara hiyo.
Amelalamikia kupunguzwa kwa kiasi kikubwa cha mgao wa idara ya mahakama, akisema huduma zake zitaimarika ikiwa itapata mgao wa kati ya Sh5 bilioni hadi Sh10 bilioni kwa mwaka.