Habari

Maseneta sasa waamua kuharakisha mswada wa kuwezesha kaunti kupata sehemu ya fedha

September 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

BAADA ya kung’amua kuwa hawataelewana haraka kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti, maseneta sasa wameafikiana kuharakisha upitishaji wa mswada utakaoiruhusu Hazina ya Kitaifa kusambaza asilimia 50 ya fedha kwa serikali za kaunti.

Kiranja wa wengi katika Seneti Irungu Kang’ata alisema Jumatatu kuwa bunge hilo linaupa mswada huo wa marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, kipaumbele litakaporejelea vikao vyake, Jumanne, Septemba 8, 2020.

“Mswada huu utashughulikiwa katika hatua ya pili na ya tatu kabla ya kupitishwa wiki ijayo,” Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge.

Mswada huo, ambao ulipitishwa katika Bunge la Kitaifa mwaka 2019 unatoa nafasi kwa Hazina ya Kitaifa kusambaza hadi asilimia 50 ya mgao wa fedha wa mwaka uliotangulia endapo Mswada wa Ugavi wa Mapato (DORA) utachelewa kupitishwa.

Mswada huo uliodhaminiwa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa unalenga kuhakikisha kuwa Serikali za Kaunti hazikabiliwi na changamoto za kifedha ilivyoshuhudiwa mwaka 2019 pale Seneti na Bunge la Kitaifa zilipochelewesha kupitishwa kwa mswada wa DORA.

Hii ni pale wabunge waliposhikilia kuwa serikali za kaunti zitengewe Sh316.5 bilioni pekee kutoka Hazina ya Kitaifa huku maseneta wakipendekeza Sh335 bilioni.

Mswada huo wa Ichungwa ulipitishwa katika bunge la kitaifa kisha ukawasilishwa kwa seneti mapema mwaka 2020.

Hata hivyo, maseneta hawajaushughulikia hadi wakati huu.

Endapo wataamua kuushughulikia kuanzia Jumanne, basi watalazimika waufanyie marekebisho ili ujumuisha Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti (CARB).

Hii ndiyo njia ya kipekee itakayowawezesha kuutumia kuziwezesha serikali za kaunti kusambaziwa angalau asilimia 50 ya fedha zilizopaswa kupata katika mwaka uliopita wa kifedha, 2019/2020.

Mvutano wa sasa kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha umezuia Seneti kupitisha mswada wa CARB utakaotoa nafasi kwa Msimamizi wa Bajeti (CoB) kuruhusu serikali za kaunti zisambaziwe sehemu ya Sh316.5 bilioni zilizotengewa katika bajeti ya mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021.