Habari

Masharti ya ibada makanisani na misikitini yalegezwa kiasi

August 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SARAH NANJALA

MAENEO ya ibada yaliyo na nafasi kubwa sasa yataruhusiwa kuwa na waumini zaidi ya 100 kwa kila ibada kulingana na nafasi iliyopo.

Pia umri wa watakaoruhusiwa kuhudhuria ibada umebadilishwa hadi zaidi ya miaka sita na chini ya miaka 65, kutoka kiwango cha awali cha kuanzia umri zaidi ya miaka 13 hadi chini ya miaka 58.

Tangazo hilo limejiri karibu mwezi mmoja baada ya maeneo ya ibada kufunguliwa tena mnamo Julai 14, huku Baraza la Makundi ya Kidini likisema uamuzi huo ulifanywa kuambatana na masharti yaliyokuwepo wakati wa awamu ya kwanza.

Akihutubia wanahabari Jumanne, mwenyekiti wa baraza hilo Askofu Anthony Muheria, alielezea kuridhika na matokeo ya kuzingatia masharti ya ibada, jambo alilosema linaashiria uongozi mzuri wa kidini.

“Baada ya kuona uzingativu wa kiwango cha juu kuhusu masharti katika sehemu za ibada, tumeshawishika kuwa Wakenya watafuata masharti hadi kiwango kifaacho,” akasema Askofu Muheria.

Mabadiliko hayo ni afueni kuu kwa viongozi wa kidini waliokuwa wamelalamikia hatua ya mwanzo ya kupunguza idadi ya waumini hadi 100 kwa kila ibada, ilhali majengo yao yangeweza kuwa na waumini zaidi.

Askofu Muheria, aliyeandamana na wanachama 14 wa baraza hilo, alieleza kuwa taifa liko tayari kwa awamu ya pili ya ufunguzi kuanzia Agosti 18.

MUDA KUONGEZWA

Awamu hiyo kando na kuwezesha maeneo ya ibada kuwa na waumini zaidi, pia itaongeza muda kutoka dakika 60 hadi dakika 90 kwa kila ibada.

Idadi itategemea umbali wa kujitenga wa mita moja unusu na nafasi iliyopo, ambapo maeneo makubwa ya ibada yataweza kuwa na watu zaidi ya 100 kwa kila ibada huku sehemu ndogo zikisalia na kiwango cha awali cha watu 100.

Haijabainika ni vipi makanisa yatachukulia masharti hayo mapya ikizingatiwa idadi ya visa vya Covid-19 vinaendelea kuongezeka.

Huku Wizara ya Afya ikiashiria kuongezeka zaidi kwa maambukizi katika majuma kadhaa yajayo, tahadhari zaidi itahitajika huku maeneo ya ibada yakiendelea kufunguliwa kwa awamu.

Licha ya ibada kuruhusiwa upya, waumini wengi wamekuwa wakiepuka kuhudhuria kwa hofu ya kuambukizwa virusi vya corona.