MASHUJAA DEI: Viongozi wahutubu kwa ukomavu
Na MWANDISHI WETU
RAIS Uhuru Kenyatta amewaongoza Wakenya kuadhimisha Sikukuu ya Mashujaa katika sherehe ya kitaifa iliyoandaliwa rasmi katika uwanja wa Gusii, Kaunti ya Kisii.
Akihutubu dakika chache baada ya saa sita mchana, kiongozi wa nchi amewasifu Wakenya wanaojitolea kufanya kazi kwa bidii jinsi tu wapiganiaji uhuru walivyofanya.
Amewataja baadhi ya viongozi wa jamii ya Abagusii waliotoa mchango muhimu katika taifa hili wakiwa ni pamoja na chifu wa cheo cha paramount wakati wa ukoloni Angwenyi Kingoina Gichana na machifu wakuu Onsongo Angwenyi, Ooga Angwenyi, Zacharia Angwenyi Ooga, Musa Nyandusi, na Assa Onyiego.
“Siku hii ilitengwa kutukumbusha kwamba historia sio tu kuhusu yaliyopita, lakini pia ni mwenge unaoangazia siku za usoni. Na hii ndiyo sababu ninawaalika leo kutafakari nami kuhusu mashujaa wa kiume na wa kike waliofafanua utaifa wetu,” amesema Rais Kenyatta.
Naibu Rais William Ruto amempongeza Rais kwa kuanzisha mpango wa kuandaa sherehe za kitaifa katika maeneo mbalimbali ya nchi tofauti na viongozi kabla yake waliozoea kuongoza sherehe za kitaifa wakiwa katika jiji kuu Nairobi.
Vile vile amejibu kauli ya kiongozi wa ODM Raila Odinga aliyesema hakuna wa kuzima mpango wa maridhiano (BBI).
Ruto amesema ni sharti wananchi wapewe fursa kujiamulia mambo muhimu.
“Tunafaa kuzungumza waziwazi kuhusu maswala yanayohusu utaifa,” amesema Ruto.