HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Mashujaa Dei yanogesha biashara Eldoret

Na WAANDISHI WETU October 20th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

BIASHARA za hoteli, Airbnb, mikahawa, teksi na uchuuzi zimepata msisimko mkubwa Eldoret huku wageni wakimiminika katika jiji hilo kuelekea kwenye sherehe za Mashujaa Dei zitakazoandaliwa leo katika Uwanja wa Kipchoge Keino.

Kuwasili kwa maafisa wa serikali, wajumbe wa kampuni na wageni wengine kumeongeza mahitaji ya malazi, chakula, usafiri na huduma nyingine, na kuwawezesha wafanyabiashara kuongeza mapato.

Edward Ambwere, ambaye hung’arisha viatu kando ya barabara ya Eldoret-Iten, alisema idadi ya wateja imeongezeka ikilinganishwa na siku za kawaida.

“Biashara ni nzuri sana kwa sasa. Kwa sababu ya wageni wengi wanaowasili jijini, tunapata wateja wengi zaidi kuliko kawaida,” akasema jana.

Agnes Chemwelo, muuzaji wa chakula karibu na Hoteli ya Silverline kwenye barabara ya Eldoret-Kapsabet, alisema sherehe hizo zimeongeza mauzo.

“Tunanufaika pakubwa na sherehe hizi. Wateja wanapoongezeka, mauzo yetu yanaongezeka pia, na hili ni baraka kwa wafanyabiashara wadogo wanaotegemea mapato ya kila siku,” akasema.

Wauzaji wa mboga pia wananufaika. Mildred Jepkoech, anayeendesha duka la mboga karibu na uwanja wa Kipchoge Keino, alisema hoteli na mikahawa inanunua bidhaa kwa wingi.

“Biashara imebadilika kabisa kuwa bora katika siku chache zilizopita. Mahitaji ya mboga yameongezeka na tunauza bidhaa zetu haraka kuliko kawaida,” akasema.

Sekta ya malazi pia inanoga huku hoteli zikishuhudia ongezeko la nafasi zilizowekwa. Absalom Chavera, meneja wa hoteli moja jijini, alisema nafasi zilianza kujaa wiki iliyopita, hasa kutokana na wageni wanaohudhuria sherehe.

Hoteli za Eka, Boma Inn, Sirikwa na Queens pia zimewapokea wageni huku Eka ikiwa imejaa tangu mwanzoni mwa Oktoba.

Wenye teksi na biashara nyingine za usafiri wanatarajiwa kunufaika kutokana na wageni wanaosafiri kati ya hoteli, uwanja na maeneo mengine ya jiji huku usalama pia ukiwa umeimarishwa.

Kamishina wa Mkoa wa Bonde la Ufa, Abdi Hassan, alisema maafisa wa usalama wametumwa katika jiji na viunga vyake kulinda wakazi na wageni kabla, wakati na baada ya sherehe.

Kaunti ya Uasin Gishu pia inatumia hafla hiyo kutangaza vivutio vyake vya utalii, ikiwemo Bwawa la Kesses , mbunga ya Mtoto Sosiani, Koromosho Falls na Eldoret Arboretum.