Masuala yaliyofuatiliwa na Wakenya katika Google Search Agosti 2019
Na CHARLES WASONGA
WATU wengi walisaka habari kuhusu mechi zilizochezwa katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Agosti, kulingana na mtandao wa Google Search ambao hutoa ripoti kuhusu masuala ambayo Wakenya husaka kwa wingi mitandaoni kila mwezi.
Mechi ambazo habari kuzihusu zilisakwa kwa wingi zilikuwa ni mtanange wa klabu ya Liverpool dhidi ya Arsenal na kipute cha Manchester United dhidi ya Chelsea.
Ilibainika kuwa Wakenya wengi bado ni waraibu wa mchezo wa kamari licha ya serikali kuzima leseni ya jumla ya kampuni 27 kwa kutolipa ushuru.
Masuala ya kamari yalikuwa ya pili kusakwa kwa wingi na Wakenya mitandaoni.
Licha ya kampuni maarufu za kamari kama vile SportPesa na Betin kuzimwa,
Wakenya bado walielekea mitandaoni kushiriki mchezo huo kupitia wavuti ya kampuni zilizosalia kama vile Bet 254, 22 Bet, Shabiki Power 17 na Odi Bet.
Kampuni ya SportPesa hata hivyo huenda ikarejelea shughuli zake baada ya masuala kadhaa kulainishwa.
Habari kuhusu kifo cha mwanamuziki maarufu John Ng’ang’a, maarufu kama John De’ Mathew mnamo Jumapili Agosti 18 ilikuwa ni ya tatu kufuatiliwa na Wakenya wengi mitandaoni mwezi huo.
Mwanamuziki huyo wa Benga ya Agikuyu alifariki baada ya kuhusika kwenye ajali katika barabara kuu ya Thika mwendo wa saa moja za jioni.
Na habari kuhusu mtoto ambaye ni mwanasarakasi zilishikilia nambari nne kama iliyofuatiliwa kwa wingi.
Hii ni baada ya madai kwamba meneja wake Joseph Mwangi Nduta alikuwa na mazoea ya kumtumia tu kujipatia pesa na ambapo mamake msichana huyo Bi Magdalene Syombua hakupata “chochote.”
Inadaiwa amefanya hivyo tangu mwaka wa 2014.
Tayari maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wameanza kumchunguza meneja huo kuhusiana na madai ya Waeni. Jumanne, Mwangi alizuiliwa kwa siku tano maafisa wa polisi wakiruhusiwa na mahakama kuendelea kumchunguza kuhusu madai kwamba aliandika barua akiifanya ionekane imetoka kwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i na kuituma kwa anwani ya baruapepe akidhamiria kumtishia Bi Syombua.
Mlinda lango wa timu ya kitaifa ya Brazil David Luiz ndiye alikuwa wa tano kufuatiliwa na Wakenya mitandaoni. Hii ni baasa ya klabu ya Uingereza Arsenal kukabilisha mpango wa kumnunua kwa pauni 8 milioni kutoka Chelsea.
Wa sita kufuatiliwa alikuwa ni bilionea na mmiliki wa kampuni ya kutengeneza mvinyo ya African Spirits, Humphrey Kariuki Ndegwa baada ya Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kuamuru akamatwe kuwa kukwepa kulipa ushuru wa kima cha Sh44.4 bilioni.
Kisa kingine kufuatiliwa kwa wingi (nambari saba) ni mkasa wa moto uliotokea katika msitu mkubwa duniani wa Amazon nchini Brazil, Amerika Kusini.
Msitu wa Amazon maarufu kama ‘Mapafu ya Dunia’ huzalisha asilimia 20 ya oksijeni ya dunia.
Msanii wa Injili, Jimmy Gait ndiye alikuwa ni katika nambari nane kufuatiliwa na Wakenya mitandaoni.
Hii ni pale alifichua kuwa madaktari wa Kenya walimpa matokeo ya kupotosha kuhusu maradhi ambayo yamekuwa yakimsibu. Alieleza kuwa angalifuata ushauri wa madaktari wa Kenya, angaliishia kupoteza sauti yake kabisa.
Hatimaye alitafuta matibabu nchini India.