• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Humphrey Kariuki aruhusiwa kusafiri ng’ambo

Humphrey Kariuki aruhusiwa kusafiri ng’ambo

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Nairobi Jumatano ilitupilia mbali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupinga bwanyenye Humphrey Kariuki kusafiri ng’ambo kuandaa biashara zake.

Hakimu mkuu Martha Mutuku alimruhusu Bw Kariuki kusafiri akisema DPP na Mahakama haziwezi kumwelekeza jinsi atakavyoendesha biashara zake.

Bi Mutuku alisema kumnyima Bw Kariuki, fursa ya kusafiri ni kukandamiza haki zake za kimsingi ikitiliwa maanani “atapata huduma za kiafya.”

Hakimu alisema DPP kupitia kiongozi wa mashtaka Bi Angela Fuchaka alishindwa kuthibitisha madai eti , mshukiwa huyo wa kesi ya kutolipa kodi ya zaidi ya Sh41bilioni kwa mamlaka ya ushuru nchini “atatoroka akiruhusiwa kusafiri.”

Bi Fuchaka alisema mshtakiwa anaweza kutumia mtandao wa Zoom kuendeleza mikutano yake na pia kutibiwa nchini kwa vile kuna watalaam wa kila tiba nchini.

“Naomba korti imnyime fursa ya kusafiri kwa vile atachana mbuga na kesi inayomkabili inahusu mabilioni ya pesa,”Bi Fuchaka alimweleza hakimu.

Lakini akitoa uamuzi , Bi Mutuku alikubaliana na wakili Cecil Miller, kwamba Bw Kariuki anayeshtakiwa pamoja na wakurugenzi wa makampuni ya kutengeneza pombe kali  ya Africa Spirits Limited (ASL) na Wow Beaverages Limited (WBL) Mbw Stuart Gerald,Peter Njenga, Robert Thinji, Simon Maundu na Kaaria Kinoti “hajakaidi maagizo ya korti ya kusafiri na kurudisha pasipoti zake mbili.”

Hakimu alisema Bw Kariuki amesafiri mara tano ng’ambo na kurudi tangu ashtakiwe miezi 14 iliyopita.

Bi Mutuku alisema kutokana na ushahidi uliopo Bw Kariuki “amesafiri mara tano na kurejesha hati zake mbili za kusafiri.”

Bw Kariuki yuko na uraia mara mbili-Kenya na Cyprus.

Mahakama ilisema katiba ya nchi hii hairuhusu haki za raia kukandamizwa na mojawapo ya haki hizo ni usafiri.

Bi Mutuku alisema mshtakiwa “amethibitisha uadilifu wake kwa kurudisha pasipoti zake mbili kwa naibu wa msajili wa mahakama anayezihifadhi.”

Hakimu huyo alisema hakuna sababu zozote zimewasilishwa na upande wa mashtaka kuthibitisha mshtakiwa “hatarudi kuendelea na kesi inayomkabili akihudhuria mikutano hiyo ya kimataifa kuhusu biashara zake.”

Akiwasilisha ombi la kutaka Bw Kariuki akubaliwe kusafiri, Bw Miller anayemtetea mshukiwa huyo katika kesi tatu za ukwepaji kulipa ushuru, alisema “mshtakiwa hana historia ya kukaidi maagizo ya korti hata siku moja. Kila anaposafiri hurudisha pasipoti na kujisalimisha kwa naibu wa msajili wa hii korti.”

Atakapokuwa ziarani ,Bw Kariuki, ataenda nchi tatu Uingereza, DRC Congo na Zambia.

Bw Kariuki na wenzake wamekana kutolipa ushuru wa zaidi ya Sh41bilioni.

Pia wamekana mashtaka ya kupatikana na kemikali inayotumika kutengeneza mfinyo kinyume cha sheria.

Pia wameshtakiwa kupatikana na leseni za ushuru zilizo na kasoro.

You can share this post!

Ulinzi Stars kupigwa jeki na marejeo ya wanasoka watatu

Neymar aandamwa na mamlaka ya ushuru Uhispania alipe Sh4.4...