Habari

Mataifa 13 yasitisha safari za Boeing 737 MAX 8

March 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na VALENTINE OBARA

MASHIRIKA ya ndege katika nchi mbalimbali, yamesitisha utumizi wa ndege aina ya Boeing 737 MAX 8, kufuatia ajali iliyotokea Jumapili nchini Ethiopia na kuangamiza watu 157 wakiwemo Wakenya 32.

Huku uchunguzi ukianzishwa kujua chanzo cha ajali ya ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Nairobi kutoka Addis Ababa, mashirika katika nchi 13 yamesitisha utumizi wa ndege hizo mara moja kwa sababu za kiusalama.

Mashirika ya ndege ya mataifa ya Uchina, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Ireland, Malaysia, Mexico, Brazil, Singapore, Australia, Cayman, Indonesia na Ethiopia yalisema hatua hiyo itadumu kwa muda usiojulikana.

Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, Meneja wa Ethiopian Airlines hapa Kenya, Bw Yilma Goshu, alisema hatua hiyo ilianza kutekelezwa Jumapili.

“Hii haimaanishi kwamba ajali ilisababishwa na muundo wa aina hii ya ndege bali ni hatua ya tahadhari huku uchunguzi ukiendelezwa. Tunalenga zaidi kushughulikia uchunguzi kwa ubora wa kimataifa mbali na kufariji na kuwapa ushauri nasaha jamaa na marafiki wa waathiriwa,” akasema.

Uamuzi wa mashirika kusitisha utumizi wa ndege hizo umetokana na kuwa hii ni mara ya pili kwa aina ya ndege ya Boeing 737 MAX 8, ambazo zilizinduliwa mwaka wa 2016, kupata ajali dakika chache baada ya kupaa.

Ajali nyingine ilitokea Oktoba mwaka uliopita Indonesia na kuua watu 180, ikasemekana kulikuwa na hitilafu ya programu za kiteknolojia.

“Tutachukua hatua zote zinazohitajika kwa usalama wa ndege zetu kabla zirudi kuhudumia wateja wetu,” Afisa Mkuu Mtendaji wa Cayman Airways, Bw Fabian Whorms akasema.

Shirika la Air China ambalo lilianza kutumia ndege za Boeing 737 MAX 8 katika mwaka wa 2017, lilisema ajali ya Ethiopia ilifanana sana na ile ya Indonesia na hivyo basi ndege hizo zitaendelea kutumiwa tu baada ya kuthibitishwa zina usalama wa kutosha.

Mashirika mengine ya ndege yalisema yanafuatilia hali ilivyo kabla yafanye uamuzi wa iwapo yatandelea kutumia ndege hizo huku ikiripotiwa bei ya hisa za kampuni ya Boeing ilianza kushuka kwa kasi jana.