Matamshi ya Ruto ni ithibati chama tawala kimelemewa – Mudavadi
Na CHARLES WASONGA
KIONGOZI wa ANC Musalia Mudavadi amekejeli Naibu Rais William Ruto kwa kudai kuwa cha Jubilee kimetekwa na matapeli.
Bw Mudavadi alisema hiyo ni ishara kwamba chama hicho tawala kimeshindwa kutoa uongozi bora kwa Wakenya, akiongeza kuwa ANC iko tayari kutekeleza wajibu huo kuanzia 2022.
“Kwa naibu kiongozi wa chama tawala kuungama kwamba kimedhibitiwa na matapeli, walaghai na wakora, inaonyesha wazi kwamba wamishindwa kusuluhisha matatizo ya wananchi walivyoahidi. Nawaambia kuwa sisi kama ANC tuko tayari kutwaa wajibu huo 2022,” Mudavadi akasema alipoongoza hafla ya kuapishwa kwa wanachama wapya wa bodi ya uchaguzi wa chama hicho Jumamosi, Nairobi.
Juzi, Dkt Ruto alikiri kuwa mambo sio shwari ndani ya Jubilee akisema migawanyiko na uhasama ndani yake imesababishwa na watu kama vile naibu mwenyekiti David Murathe, aliowataja kama “matapeli na wakora”.
Bw Mudavadi alisema kuzinduliwa kwa bodi hiyo ya uchaguzi ni sehemu ya maandalizi ya ANC kwa uchaguzi mkuu ujao ambapo atawania kiti cha urais.
Bodi hiyo, ambayo itaongozwa na Salim Busaidy kama mwenyekiti, itaandaa na kusimamia na kuendesha uteuzi wa wagombeaji watakaogombea nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi huo ambao utafanyika mwaka wa 2022.
Aidha, itaandaa sajili ya wanachama ambao watahitimu kushiriki katika mchujo na uchaguzi wa maafisa wapya wa chama hicho.
“Mtatekeleza wajibu wa kutuwezesha kuendesha uchaguzi wa maafisa wapya katika ngazi zote na uteuzi wa wale ambao watapeperusha bendera ya chama chetu katika uchaguzi mkuu ujao,” Bw Mudavadi akawaambia wanachama wa bodi hiyo.
Mbunge Maalum Godfrey Osotsi na wanachama wengine wa ANC wamekuwa wakimtaka Bw Mudavadi kuitisha uchaguzi wa maafisa wapya wa chama ambapo muda wa hatamu ya maafisa wa sasa umekamilika.
Juzi, ANC ilipata pigo kufuatia kujiuzulu kwa Katibu Mkuu Barrack Muluka na aliyekuwa mgombea wake katika uchaguzi mdogo wa Kibra mwaka 2019, Bw Eliud Owalo.