Matatu yagonga bodaboda na abiria kabla ya kuangukia mpita njia na kuwaua
WATU watatu wameangamia Jumapili na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali ya barabarani eneo la Keroka, mji unaopakana na kaunti za Kisii na Nyamira.
Ajali hiyo ilihusisha matatu aina ya Nissan iliyokuwa ikielekea Keroka kutoka Masimba na pikipiki.
Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Trafiki Kaunti Ndogo ya Masaba Kaskazini, Peter Chege, dereva wa matatu hiyo alipoteza udhibiti wa gari lake alipokuwa akishuka kwenye barabara ya Ichuni. Wakati akihangaika kulidhibiti gari lake, alimgonga mwendesha pikipiki aliyekuwa mbele yake, na kumuua pamoja na abiria wake. Kisha matatu hiyo ilitua kwenye mtaro uliokuwa karibu na kumwangukia mpita njia mmoja ambaye pia aliangamia papo hapo.
“Watu watatu walipoteza maisha yao, na wengine kadhaa kujeruhiwa. Wale walio na majeraha mabaya wamekimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH) na hospitali zingine ndani ya Keroka,” Bw Chege aliambia Taifa Leo kwa simu.
Kufuatia ajali hiyo, Mwenyekiti wa Bodaboda Kaunti Ndogo ya Masaba Kaskazini, Dominic Babu alitoa wito wa kuhamishwa kwa wafanyabiashara ambao alisema wanauza bidhaa karibu mno na barabara hiyo.
“Wafanyabiashara katika barabara hiyo wamejenga vibanda karibu na barabara kuu na kuna haja ya kuwadhibiti ikiwa tutaepuka ajali kama hizi siku zijazo,” Bw Babu alisema.
Pia aliomba Mamlaka ya Kitaifa na Barabara Kuu za Kenya (Kenha) kuweka alama mpya za barabarani ili kuwaonya madereva na watumiaji wengine wa barabara.