Habari

Matiang’i aonya kampuni za uchezaji kamari

June 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RUTH MBULA

WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i amesema kuwa leseni za kampuni nyingi za uchezaji kamari hazitatolewa upya baada ya mchakato wa upigaji msasa unaoendelea kukamilika.

Jumamosi, waziri huyo alisema kuwa tayari amepokea ripoti maalum kutoka kwa Bodi ya Kudhibiti Uchezaji Kamari (BCLB) na anaitathmini. Alisema kuwa kampuni nyingi hazijakuwa zikilipa kodi.

“Lazima kampuni zote zizingatie sheria,” akasema Matiang’i.

Alisikitika kuwa vijana wengi hawajakuwa wakitumia muda wao kikamilifu, wakijihusisha na kamari.

Mbali na hayo, alisema kuwa visa vya vijana kujitoa uhai vimeongezeka nchini kutokana na athari za uraibu huo.

“Hatuwezi kuwa nchi ya uchezaji kamari. Lazima tuishi maisha ya kikweli. Vijana wengi hufadhaika sana wanapokosa kufanikiwa wakicheza kamari,” alisema Dkt Matiang’i, alipohutubu katika Kanisa la SDA Mekonge, Kaunti ya Kisii, alikohudhuria ibada.

“Hapa Kisii, idadi ya visa vya watu kujitoa uhai ni ya kusikitisha,” alisema.

Ukweli

Alieleza kuwa umefika wakati kwa Wakenya kuelezwa ukweli, kwamba uchezaji kamari hauna manufaa yoyote katika ukuaji wa uchumi.

Wakati huo huo, Dkt Matiang’i ameapa kuhakikisha kuwa Sh450 bilioni ambazo zilitengewa miradi ya maendeleo katika bajeti ya mwaka 2019/2020 zimetumika kama ilivyokusudiwa.

Aliwaagiza makamishna wa kaunti kuhakikisha kuwa wakandarasi wazembe, ambao hawamalizi kazi walizotengewa wamekamatwa na kushtakiwa, kwani wanachelewesha malengo ya maendeleo ya serikali.

Alikuwa ameandamana na Gavana James Ongwae (Kisii) naibu wake Joash Maangi, wabunge Jimmy Angwenyi (Kitutu Chache Kaskazini), Richard Onyonka (Kitutu Chache Kusini) na madiwani kadhaa.