Habari

Mawakili 35 waenda kortini kupinga kufurushwa kwa familia zinazoishi ndani ya msitu wa Mau

August 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VITALIS KIMUTAI na CHARLES WASONGA

MPANGO wa serikali wa kufurusha familia zinazoishi ndani ya msitu wa Mau sasa umepingwa na mawikili 35 maarufu kutoka Rift Valley ambao wamewasilisha kesi mahakamani.

Wakiongozwa na wakili wa Nairobi Moses Kurgat na Hillary Sigei pamoja na mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) tawi la South Rift Kipngetich Korir, mawakili hao wanataka mahakama kusitisha ufurushaji huo hadi kesi yao itakaposikizwa na kuamuliwa.

“Wakazi na hasa watoto ambao hawana ufahamu kuhusu suala hili wataathiriwa na maisha yao kuvurugwa ikiwa washtakiwa wataendelea na awamu ya pili ya ufurushaji,” mawakili hao wanasema katika kesi yao.

Jaji wa Mahakama ya Masuala ya Mazingira na Ardhi Silas Munyao ameamuru kwamba kesi hiyo isikizwe mjini Kitale mnamo Jumatano wiki ijayo.

Agizo la mahakama limewasilishwa kwa watu 11 wanaotajwa kama washtakiwa katika kesi hiyo.

Kesi hii mpya inajiri huku kesi nyingine iliyowasilishwa na Gavana wa Kericho Paul Chepkwony kupinga ufurushaji huo ikiwa ingali kusikizwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu Haki na kitengo cha Mazingira na Ardhi katika Mahakama Kuu ya Narok.

Katika kesi yao, mawakili hao wanataja shule za msingi 16 katika eneo hilo ambazo wanasema zitaathiriwa ikiwa serikali itaendelea na ufurushaji huo ambapo zaidi ya wanafunzi 10,000 hawatakuwa na pa kusomea.

Baadhi ya shule hizo ziko katika wadi za Ololulunga, Melelo, Sogoo na Segemian katika Kaunti ya Narok.

Eneo ambako ufurushaji utatekelezwa limepanuliwa ili kujumuisha shule zingine 15 za msingi.

Serikali imesisitiza kuendeleza mpango wa utunzaji na uhifadhi wa msitu huo wa Mau ambao ni mojawapo ya chemichemi tano za maji nchini Kenya.

Inaelekezewa lawama kwa kufurusha watu kutoka ardhi ambayo walinunua na kupewa stakabadhi husika za umiliki.

Njia panda

Ufurushaji huo pia huenda ukamweka Naibu Rais Wiliam Ruto pabaya machoni mwa wakazi kuhusu ikiwa ataunga mkono hatua ya serikali au atatetea wakazi wa eneo hilo ambalo ni ngome yake ya kisiasa.

Haya yanajiri wakati ambapo kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM) Isaac Ruto akiamua kuongoza mazungumzo na serikali na wadau wengine kwa lengo la kusitisha ufurushaji huo.

Katika awamu ya kwanza ya shughuli hiyo iliyotekelezwa miaka 14 iliyopita katika eneo la Narok Kusini, shule 15 zilibomolewa na maafisa wa usalama waliotwikwa wajibu wa kuwaondoa waliokuwa wamepenyeza na kuanza kuishi ndani ya ngome ya msitu huo.

Aliyekuwa Waziri wa Elimu marehemu George Saitoti alitangaza wakati huo kwamba serikali ilikuwa imetoa Sh4.9 milioni kwa mpango wa elimu bila malipo kufaidi zaidi ya wanafunzi 1,449 ambao wazazi wao walihamishwa makwao katika operesheni hiyo.

“Jumla ya walimu 70 walioajiriwa na Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) watatumwa katika shule zingine kufuatia kuhamishwa kwa zaidi ya familia 10,000 wakiwemo zaidi ya wanafunzi 3,000,” akasema Profesa Saitoti wakati huo.