HabariSiasa

Mawaziri kutua magharibi siasa zikipamba moto

July 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DERICK LUVEGA

UJUMBE wa serikali ukiongozwa na mawaziri watano unatarajiwa kufanya ziara ya siku mbili katika eneo la Magharibi kuanzia Jumatatu.

Ziara hiyo inatokea wakati ambapo kuna mvutano wa kisiasa baina ya viongozi wa magharibi, upande mmoja ukiunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Riala Odinga, huku upande mwingine ukiegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.

Hivi majuzi, Rais Kenyatta aliagiza mawaziri wawe wakienda mashinani kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.Mawaziri watakaoongoza ujumbe huo ni Peter Munya (Kilimo), John Munyes (Madini), Sicily Kariuki (Maji), James Macharia (Uchukuzi) na Mutahi Kagwe (Afya).Ujumbe huo wa serikali utazuru Kaunti za Kakamega, Trans Nzoia, Busia, Vihiga na Bungoma.

Waziri wa Kilimo atazuru Kiwanda cha Sukari cha Mumias ambacho kinakumbwa na masaibu tele, ikiwemo kukatiwa umeme kwa kushindwa kulipia huduma hiyo.

Maafisa wa wizara ya Kilimo pia watakagua Kiwanda cha Sukari cha Nzoia katika Kaunti ya Bungoma. Baadaye, ujumbe huo wa serikali utafanya kikao na viongozi kutoka eneo hilo kabla ya kuhutubia wanahabari kuhusu mikakati ya kuboresha sekta ya sukari.

Waziri wa Afya Bw Kagwe pia atahutubia taifa kuhusu hali ya maambukizi ya virusi vya corona kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kakamega baada ya kuzuru Hospitali ya Rufaa ya Trans Nzoia leo asubuhi.

Kesho, Bw Kagwe atahutubia taifa kutoka Kaunti ya Busia ambayo ni miongoni mwa maeneo yaliyo na idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona.

Maafisa wa Wizara ya Uchukuzi wakiongozwa na Bw Macharia watazuru uwanja mdogo wa ndege wa Kakamega ambapo shughuli ya ukarabati inaendelea.

Baadaye, Waziri Macharia pamoja na kikosi chake wataelekea katika uwanja mdogo wa Nangina ulioko katika Kaunti ya Busia.

Waziri Macharia pia atakagua shughuli ya ukarabati inayoendelea katika barabara za Busia-Malaba, Kakamega-Navakholo-Musikoma, Chepsonoi, Kitale-Suam-Endebess-Kwanza, Gisambai-Shamakhokho –Musena, Ekwanda-Luanda-Esirulo-Magada na atazindua ujenzi wa barabara ya Misikhu-Brigadier.

Waziri wa Kilimo Bw Munya, kesho atazuru Chuo Kikuu cha Alupe ambapo anatarajiwa kukutana na Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong na viongozi wengineo wa eneo hilo kujadili mikakati ya kufufua kilimo na viwanda vya pamba.

Gavana Wycliffe Oparanya ambaye ni mwandalizi wa mikutano hiyo, alithibitisha ziara hiyo ya maafisa wa serikali.

Ziara hiyo inafuatia miezi miwili tangu Gavana Oparanya na Waziri wa Ugatuzi Eugine Wamalwa ‘kutawazwa’ kuwa wasemaji wa jamii ya Waluhya ambao watafanya mazungumzo na serikali kuu ili kuhakikisha kuwa eneo la Magharibi linanufaika na miradi ya maendeleo, ikiwemo kufufua sekta ya sukari na kilimo cha pamba.

Katika Kaunti ya Vihiga, waziri wa Maji atakagua na kuzindua mradi wa maji wa Sh1.7 bilioni unaofadhiliwa na serikali ya Ubelgiji. Waziri wa Maji pia atazindua mradi wa maji wa Kiptogot Kolongolo katika Kaunti ya Trans-Nzoia.

Waziri Munyes ataongoza hafla ya kukabidhi rasmi kiwanda cha mawe ya matale kutoka kwa serikali ya Kaunti hadi Serikali ya Kitaifa.

Bw Oparanya jana alisema kuwa ziara ya mawaziri hao ni ishara kwamba Rais Kenyatta ana azma ya kukamilisha miradi yote iliyokuwa imekwama katika eneo la Magharibi.