Mbarire ataka Gachagua azuiwe kufanya kampeni Mbeere Kaskazini
UDA sasa inataka Kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua azuiwe kufanya kampeni Mbeere Kaskazini kuelekea uchaguzi mdogo wa Novemba 27.
Mwenyekiti wa UDA, Cecily Mbarire, alisema aliyekuwa naibu rais hafai kukanyaga Mbeere Kaskazini kwa sababu DCP haina mwaniaji huko.
Akiwa ameandamana na wakili Andrian Kamotho, Bi Mbarire ambaye pia ni Gavana wa Embu, alisema kuwa DCP haikutia saini mwongozo wa uchaguzi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini kwa hivyo hafai kuendeleza shughuli zozote za kisiasa Mbeere Kaskazini.
Pia Bi Mbarire aliitaka IEBC imzuie Bw Gachagua kuendesha kampeni kwa mwaniaji wa DP Newton Kariuki maarufu kama Newton Karish.
Aidha, alidai kuwa aliyekuwa naibu rais anapanga kuwatumia wahuni kuzuia ghasia wakati wa kampeni za kisiasa eneo la Mbeere Kaskazini.
“Anawatoa wahuni kutoka Kayole, Nairobi na Kirinyaga waje Mbeere Kaskazini ili kuzua ghasia kisha walaumu UDA,” akasema baada ya kuandikisha taarifa katika kituo cha polisi.
“Tumewapo polisi majina ya wale ambao wanataka kutumiwa kuzua ghasia Mbeere Kaskazini. Sisi hatupangi kutumia ghasia zozote wakati ambapo tunasaka kura kwa sababu sisi si chama cha fujo,” akasema Bi Mbarire.