Mbunge akerwa na walimu kuwafukuza wanafunzi akidai wana tamaa ya pesa
WALIMU kutoka Mumias Magharibi Kaunti ya Kakamega wamekashifiwa na mbunge wa eneo Johnson Naicca akidai ni wazembe na wamechangia matokeo duni kwenye mitihani ya kitaifa.
Bw Naicca ameonekana pia kukerwa na kufukuzwa kwa watoto mara kwa mara kutokana na ukosefu wa karo akisema walimu wana tamaa na wanaipa kipaumbele pesa kuliko kuwasomesha watoto.
“Hawa walimu wana tamaa ya pesa kuliko kutekeleza jukumu lao la kufundisha. Wanalipwa mshahara na serikali ilhali bado wanaotea pesa za wazazi ndiyo maana wanawafukuza watoto mara kwa mara,” akasema mbunge huyo.
Alisema hataendelea kuwavumilia walimu wakuu kuwafukuza watoto huku akisisitiza serikali imekuwa ikiwajibika kwa kutuma pesa shuleni na wakuu hao wanastahili kutumia pesa hizo.
Kando na pesa za kufadhili elimu ya watoto, mbunge huyo alisema Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge Nchini (CDF) imekuwa ikitoa pesa kwa shule za eneo hilo kugharimia mahitaji ya watoto shuleni.
“Tumetenga asilimia 40 ya CDF kufadhili elimu, tunayajenga madarasa, maabara, maktaba na vyoo. Pia huwa tunatoa basari kwa wanafunzi kutoka familia zisizojiweza,
“Licha ya haya yote baadhi ya walimu wanaendelea kutuhangaisha kwa kuwafukuza wanafunzi na mwishowe wanafunzi kuyapata matokeo duni kwenye mitihani ya kitaifa,” akaongeza.
Mwanasiasa huyo anayehudumu muhula wake watatu alisikitika kuwa wengi wa wanafunzi ni mayatima na wanaishi na walezi ambao ni wakongwe kwa hivyo hata wakitumwa nyumbani, huwa hawapati karo.
Aliwataka walimu wakuu wakubali wazazi wasiokuwa na pesa walete kuni, mahindi, maharagwe au bidhaa nyingine shuleni badala ya kuwatuma wanafunzi nyumbani kisha kusisitiza wanataka pesa tu.
Mwenyekiti wa Muungano wa Walimu Wakuu Kaunti ya Kakamega Francis Amukowa hata hivyo aliwatetea walimu wakuu, akisema mara nyingi huwa hawana jingine ila kuwafukuza wanafunzi kutokana na kucheleweshewa pesa za ufadhili wa elimu kutoka serikali kuu.
“Shule zinaandamwa na madeni na wasimamizi huwa hawana jingine ila kuwatuma wanafunzi nyumbani walete hela,” akasema Bw Amukowa.