HabariSiasa

Mbunge wa kike ajitolea kuwafunza wanaume mbinu za kutongoza

December 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PIUS MAUNDU

MBUNGE Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Makueni, Bi Rose Museo, amejitolea kuwafunza wanaume jinsi ya kutongoza wanawake wa umri wao ili kesi za unajisi ambazo zimekuwa zikiongezeka katika kaunti hiyo zipungue.

“Niko tayari kudhamini semina za kufundisha wanaume jinsi ya kutongoza wanawake wa umri wao ili waachane na watoto,” alisema.

Alikuwa akizungumza katika Soko la Kisayani, Kibwezi mwishoni mwa wiki ambapo aliunga mkono viongozi ambao wamelalamika kuhusu uovu huo.

Wadau wengi wameelezea wasiwasi wao baada ya watu zaidi ya 10 kuhukumiwa kifungo cha maisha na kadhaa kufungwa kwa hadi miaka 20 katika korti za Makueni mwezi uliopita kwa unajisi, ubakaji na ulawiti.

 

Hapo awali, Bi Museo alifanya vikao na machifu na manaibu wao pamoja na polisi kuhusu namna ya kupambana na makosa ya dhuluma za mapenzi.

Alihusisha visa vya ubakaji na matumizi ya dawa za kulevya na tabia ya ‘kujinyamazia’ miongoni mwa wahusika katika mikutano iliyofanywa miezi mitatu iliyopita.

Wakati huo huo, Kamishna wa Kaunti ya Makueni, Bw Mohammed Maalim, aliwalaumu machifu na polisi kwa kuzembea kazini akiwaonya vikali dhidi ya kutatua kesi za unajisi nje ya mahakama.

Kwa mujibu wa Bi Monicah Owenga, ambaye ni mwakilishi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma katika kaunti hiyo, kucheleweshwa kwa kesi za aina hiyo kumekiuka haki za waathiriwa.

Alisema ongezeko la visa vya ubakaji kumechangia kuongezwa kwa mahakimu watatu katika korti za Makindu mnamo Oktoba. Korti ya Makindu huhudumia maeneo ya Kibwezi na Nzaui.

Mahakimu Bw Sitati Temba (Lamu), Bw Edward Too (Moyale) na Bw Charles Mayamba (Kilungu) walifanya kazi kutoka korti za Makindu kwa wiki tatu chini ya mpangilio maalum iliofadhiliwa na Bi Museo kusaidia kupunguza kurudisha nyuma kwa kesi zaidi ya 200 za unajisi ambazo zilikuwa zimecheleweshwa tangu 2014.

Wamesaidia hakimu mkuu wa mahakama ya Makindu Bw Jared Magori na mahakimu waandamizi Bi Damaris Karani na Bi Annastacia Ndung’u.

Wale waliotiwa gerezani katika kipindi hicho ni pamoja na waendeshaji bodaboda, wachungaji, wafanyakazi wa mashamba, walimu na wafanyabiashara.

Serikali ya kaunti imeanzisha kituo cha waathiriwa wa tuhuma za unyanyasaji wa kimapenzi katika Hospitali ya Rufaa ya Makueni kwa kushirikiana na Hospitali ya Wanawake ya Nairobi.

Imeandaa kwa pamoja mikutano na mahakama za Kilungu katika Soko la Nunguni kuhamasisha jamii kuhusu dhuluma za kimapenzi.