Mfanyabiashara hatarini kupoteza magari, Sh34 milioni
MFANYABIASHARA huenda akapoteza mali ya zaidi ya Sh34 milioni na magari mawili ya kifahari kwa kuhusishwa na biashara ya utakasaji wa pesa haramu, kwa Kimombo money laundering.
Mahakama imeamrisha Anthony Kepha Odiero arejeshe pesa hizo na magari mawili kwa serikali baada ya kushindwa kueleza alikotoa hela hizo nyingi.
“Odiero hajaeleza kulikotoka pesa hizo. Pia hajabainisha washirika wake wa kibiashara na akaunti ambazo anadai alilipwa pesa taslimu haziko Kenya,” akasema Jaji Patrick J Otieno.
Jaji Otieno alishangaa jinsi Bw Odiero alikuwa akisafiri hadi Ulaya na Asia kuchukua pesa taslimu kisha anarejea nchini kuweka pesa hizo kwenye benki.
“Kama hiyo ndiyo hali, basi hakuziambia asasi husika kulikotoka pesa hizo na kama zilikuwa za nini. Hata kama hivyo ndivyo ingekuwa hali, bado jinsi alivyopata pesa hizo ingezua shaka,” akaongeza Jaji.
Mamlaka ya Kutwaa Mali iliyopatwa Kiharamu (ARA) ilisema walifanya uchunguzi kuhusu madai ya ulanguzi wa fedha na dawa za kulevya dhidi ya Bw Odiero na walipata kuwa mali yake nyingi ilipatikana kwa njia haramu.
ARA ilisema Bw Odiero alikuwa akiweka pesa kidogo hasa chini ya Sh1 milioni ili asigunduliwe. Ingawa ARA ilikiri kuwa haikufahamu mahali pesa hizo zilitokea, iliafikia uamuzi kuwa zilipatikana kwa njia haramu.
Pesa hizo ziliwekwa katika benki kati ya 2020 na 2023 ambapo jumla ya Sh77 milioni ziliwekwa. Alipoulizwa pesa hizo zilikotoka, alisema alizipata kwa kutangamana na watu wenye ushawishi wanaoshikilia nyadhifa za juu katika serikali za mataifa mbalimbali ulimwenguni.