Mgao kwa sekta ya kilimo wadidimia
Na JULIUS SIGEI
KWA miaka mingi, kilimo kiliaminika kuwa uti wa mgongo wa Kenya.
Hata hivyo, huenda huo si ukweli kwa serikali, ambayo imeamua kuitengea sekta hiyo Sh52 bilioni pekee kwenye bajeti.
Hilo lilikuwa ni ongezeko la asilimia 0.3 pekee kutoka Sh45 bilioni mwaka wa kifedha wa 2018/2019.
Kulingana na ripoti ya serikali, kilimo huchangia asilimia 34 ya mapato yote nchini, huajiri asilimia 70 ya wananchi na huchangia asilimia 80 ya bidhaa zote zinazouzwa nje kutoka nchini.
Hivyo, mgao huo ni kinyume cha mkakati wa kufufua na kukuza sekta ya kilimo 2019-2029, ambao kulingana na serikali, ni njia wazi ya kukabiliana na baa la njaa ya mara kwa mara nchini.
Mojawapo ya mapendekezo katika mkakati huo ni kuanzishwa kwa mashamba 50 ya ekari 2,500 kila moja au zaidi katika mpango wa kutumia ekari 500,000 kwa kilimo nchini.
Ingawa mpango huo unatekelezwa na kumilikiwa na sekta ya kibinafsi, haibainiki jinsi mgao wa sasa utasaidia katika utekelezaji wa mpango huo.
Kwa sasa, wananchi wanakabiliwa na njaa kutokana na upungufu wa mahindi nchini kwa sababu ya mazao ya chini kutokana na upungufu wa kiwango cha mvua na usimamizi mbaya wa mauzo ya zao hilo nchini. Kenya hununua kiwango kikubwa cha vyakula vingine nje ya nchi kwa sababu ya kutegemea sana kilimo kinachotegemea mvua.
Bajeti
Katika taarifa ya bajeti iliyowasilishwa Alhamisi bungeni na Waziri wa Kilimo Henry Rotich, mgawo wa unyunyiziaji maji mashamba na programu za kutengeneza mashamba ulipunguzwa pakubwa katika bajeti hadi Sh865 milioni.
Isitoshe, Sh752 milioni zilipunguzwa kutoka mgawo wa ukuzaji na usimamizi wa mazao. Vile vile, idara hiyo ilipunguziwa Sh972 milioni katika bajeti ya kufanya utafiti.
Mwaka jana, mahitaji ya ngano nchini yalikuwa ni tani milioni mbili licha ya uzalishaji wa tani 336,000 pekee nchini. Mahitaji ya mchele yalikuwa ni tani 706,000 dhidi ya uzalishaji wa tani 112,000.
Na asilimia 80 ya viazi ambavyo hutumiwa Nairobi hutoka Tanzania kulingana na wataalam katika sekta hiyo.
Hivyo, huenda hali ya upungufu wa bajeti ikawa mbaya zaidi kutokana na hatua ya serikali kuanza tena kutoza ushuru aina ya VAT kwa mbolea na dawa za kunyunyizia mimea.
“Ni muhimu kukabiliana na mwenendo mbaya ambapo mgawo wa bajeti ya kilimo na chakula unazidi kupungua,” lilisema shirika lisilo la kiserikali, Route to Food kwenye taarifa.