Habari

MGOMO: Serikali yavuna matunda ya kukaidi mahakama

February 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

UJASIRI wa wauguzi wa kukaidi agizo la Rais Uhuru Kenyatta Jumatano na kuendelea na mgomo wao, unaonyesha mtindo mbaya wa kukaidi maagizo ya mahakama na mamlaka nchini, ambao Serikali ilianzisha yenyewe.

Hapo Jumatano, Rais Kenyatta aliwaambia wauguzi kwamba iwapo hawatarudi kazini kufikia Ijumaa watafutwa kazi, akisema mgomo wao ni haramu kwani mahakama ilikuwa imetoa agizo la kusitishwa kwa mgomo huo hadi juhudi za upatanishi zikamilike.

Licha ya kuwaambia kwamba yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi nchini, muda mfupi baadaye wauguzi waliapa kwamba hawatarudi kazini hadi waongezewe marupurupu waliyoahidiwa 2017.

Maafisa wa Chama cha Wauguzi (KNUN) wakiongozwa na Katibu Mkuu, Seth Panyako, walikuwa na ujasiri wa kumkaidi Rais na kumwambia ni haki yao ya kikatiba kugoma: “Mgomo bado upo na unaendelea hadi tutakapotoa mwelekeo tofauti,” alisema Bw Panyako.

Kauli ya wauguzi ilionyesha kukomaa kwa matunda ya mtindo wa serikali yenyewe kupuuza mahakama, ambao imekuwa ikionywa kuwa ni mbegu mbaya kwa utawala wa sheria.

Mtindo huu wa kukaidi mamlaka na hasa mahakama ulipewa msingi na maafisa wakuu wa serikali., ambao wamekuwa msitari wa mbele kukaidi maagizo ya mahakama, jambo ambalo majaji wakiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga wamekuwa wakisisitiza limetoa mfano mbaya kwa wananchi nao kupuuza mahakama na mamlaka nyingine za kisheria.

Mnamo Januari 30 mwaka jana, Serikali ilipuuza agizo la mahakama la kurejesha hewani televisheni ilizozima kwa kupeperusha moja kwa moja hafla ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga alikijiapisha kama rais wa wananchi katika Uhuru Park.

Mwaka jana pia, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiangi, Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinnet na Katibu wa Wizara Gordon Kihalangwa walikaidi agizo la mahakama lililowataka wamrudishie wakili Miguna Miguna paspoti yake ili aweze kuingia nchini.

Kufuatia kupuuzwa huko kwa agizo la korti, Jaji George Odunga alisema hakuna afisa wa serikali aliye juu ya sheria.

“Hakuna kinga kwa wanaokosa kutii sheria, wakati umefika mahakama ziwafichue wale wanaokosa kuitii. Hakuna mtu aliye juu ya sheria. Maafisa wa serikali hawawezi kuruhusiwa kutembea kwa madaha huku wakikaidi maagizo ya korti,” Jaji Odunga alisema alipoagiza Bw Miguna kufikishwa kortini, agizo ambalo halikutekelezwa na badala yake akafurushwa nchini.

Mnamo 2016, Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho alihukumiwa miezi mitatu jela kwa kukataa kutii agizo la kumlipa fidia mwathiriwa aliyeteswa na serikali. Hata hivyo hakutumikia hukumu hiyo.

Jaji Odunga alikuwa amemwagiza Bw Boinnet kumkamata Bw Kibicho na kumpeleka jela kwa kukaidi agizo la kumlipa Michael Danson Mahugu fidia ya Sh2.6 milioni.

Mwaka huo huo, Jaji John Mativo aliwapata makatibu wa wizara za uchukuzi na ardhi na hatia ya kukaidi mahakama na akawahukumu kufungwa jela miezi sita. Hukumu hiyo haikutekelezwa.

Wawili hao walikuwa wamekaidi agizo la kumlipa Wilson Kamau Maina fidia ya Sh349,957 kwa majeraha ambayo mama yake Bilha Wangui Maina alipata kwenye ajali iliyohusisha gari la serikali.

Agizo lingine la mahakama ambalo serikali ilikaidi ni la kutoongeza muda wa kuhudumu wa aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa Bodi ya Kusimamia Mashirika Sasiyo ya Kiserikali, Fazul Mohamed. Baada ya agizo hilo kutolewa 2017, Bw Fazul aliendelea kuhudumu.

Mnamo 2016, Jaji Mativo akihudumu Nyeri aliagiza makatibu watano wa wizara John Mosonik ( miundomisingi), Wilson Irungu (uchukuzi), Mariamu El Maawy (ardhi ), Aidah Munano ( makao) na Paul Mwangi ( ujenzi) kutumikia hukumu ya miezi sita jela kwa kukaidi agizo la mahakama. Hata hivyo hawakutumikia hukumu hiyo.