Mhariri kutoka Tanzania Maria Sarungi aachiliwa huru baada ya kutekwa Kenya
MHARIRI na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Tanzania Maria Sarungi Tsehai aliyetekwa nyara Jumapili mchana jijini Nairobi amechiliwa huru.
Rais wa Chama Cha Wanasheria Kenya Faith Odhiambo alitangaza kuachiliwa kwa Bi Sarungi Jumapili usiku kupitia anwani yake ya X na kuambatisha picha na video akiwa na mhariri huyo na watetezi wengine wa haki za binadamu.
Katika video fupi, Bi Sarungi anashukuru wote walioshinikiza aachiliwe huru na kusema atashukuru zaidi wote waliochochea kuachiliwa kwake Jumatatu.
Mashirika ya na watetezi wa haki za kibinadamu wamelaani kutekwa nyara kwa Mhariri na mtetezi wa haki za binadamu raia wa Tanzania Maria Sarungi Tsehai.
Maria aliripotiwa kutoweka baada ya kutekwa nyara jijini Nairobi, Kenya mnamo Jumapili.
Shirika la Amnesty International Kenya, katika taarifa yake, ilidai kuwa Sarungi alitekwa nyara Jumapili mchana.
“Maria Tsehai, mhariri wa habari huru wa Tanzania na mtetezi wa haki za binadamu, alitekwa nyara na watu watatu waliokuwa na silaha ambao walitumia gari nyeusi aina ya Noah akiwa Chaka Place, Kilimani, Nairobi, saa tisa na robo,” shirika hilo lilisema.
Sarungi amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Tanzania na utawala wa Rais Samia Suluhu.
Alitorokea Kenya mwaka wa 2020 kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania uliokumbwa na utata na amekuwa akiendesha Chanzo TV, jukwaa la mtandaoni linalohimiza demokrasia.
Ripoti za kutekwa nyara kwake zimeibua hasira, huku kiongozi wa upinzani Tanzania, Tundu Lissu akilaani tukio hilo na kuwataka Wakenya kuingilia kati.
“Mpinzani mkubwa wa udikteta wa Magufuli, Maria alienda uhamishoni nchini Kenya kabla ya uchaguzi wa 2020 uliokumbwa na udanganyifu. Ni lazima tuwaambie wale waliohusika na utekaji nyara wake kwamba hakuna kiasi chochote cha ugaidi au vurugu kitakachotunyamazisha. Akina Maria wengi zaidi watainuka kupigania demokrasia nchini Tanzania,” alisema Lissu.
Kiongozi wa Chama cha NARC-Kenya Martha Karua pia alikashifu utekaji nyara huo, akiishtumu serikali ya Kenya kwa kuhusika.
“Ninalaani kitendo hiki cha uhalifu na kisicho cha kibinadamu, ambacho kimekuwa alama ya utawala mbovu wa Ruto. Nataka Maria aachiliwe mara moja na bila masharti,” Karua alisema.
Seneta wa Busia Okiya Omtatah alitaja tukio hilo kuwa ukiukaji mkubwa wa uhuru wa kibinafsi, akililinganisha na kutekwa nyara kwa kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye hivi majuzi.
“Tukio hili, linalofuatia utekaji nyara wa Kizza Besigye, ni ukiukaji wa haki za binadamu. Linaleta wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa watu binafsi ndani ya mipaka yetu.”
Alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuishinikiza serikali ya Kenya kuhakikisha kuwa Sarungi anaachiliwa na kuwalinda raia na wakazi wote kutokana na vitendo hivyo.