Habari

Miaka 57 bila madaraka

June 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyetta Jumatatu anaongoza Wakenya kuadhimisha Siku Kuu ya 57 ya Madaraka Dei, raia wakiwa wangali wanakabiliwa na maadui watatu wakuu ambao watangulizi wake akiwemo rais wa kwanza Mzee Jomo Kenyatta walikosa kuangamiza.

Maadui hawa ni umaskini, magonjwa na ujinga, ambayo waliochukua uongozi kutoka kwa mkoloni waliahidi kutatua.

Lakini miaka 57 baadaye, Wakenya wanakufa kwa kwa maelfu kila mwaka kutokana na maradhi kama numonia, kansa na malaria.

Njaa nayo inaumiza mamilioni ya watu maskini kutoka Turkana hadi Kwale huku idadi kubwa ya watoto wakiacha shule kwa kukosa karo kutokana na umaskini.

Ingawa Kenya imepiga hatua kimaendeleo tangu 1963 ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza, wataalamu wa uchumi wanasema ni kundi la wachache linalojivunia madaraka ya kuimarika kwa viwango vya juu vya maisha, huku mamilioni wakibaki katika lindi la umaskini.

Wanauchumi hao wanawalaumu viongozi kwa kuendeleza kasumba ya kuwagawanya Wakenya katika matabaka mawili makuu ya maskini na matajiri.

“Filisofia ya wa uongozi wa Kenya ni kuwa maskini waendelee kuwa maskini na matajiri waendelee kutajirika zaidi. Hii ndiyo sababu pengo kati ya matajiri na maskini linaendelea kupanuka na viongozi wanahakikisha hali imebaki hivi kimakusudi,” asema mwanaharakati Swaleh Mohammed.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Afrobarometer, viwango vya umaskini nchini Kenya viliongezeka kati ya 2014 na 2018 ingawa vilikuwa vimepungua miaka minne iliyotangulia.

Kulingana na ripoti hiyo, karibu nusu ya Wakenya hawapati chakula cha kutosha huku 55 wakikosa huduma bora huduma za matibabu.

Ripoti ya Benki ya Dunia mwaka jana ilionyesha kuwa viwango vya umaskini nchini Kenya bado vinaendelea kuongezeka.

Wataalamu wa uchumi wanasema ingawa serikali imeweka mikakati ya kupigana na magonjwa na umasikini, utawala mbaya, ufisadi, ukabila na tamaa ya viongozi zinavuruga malengo haya.

“Tangu Kenya ilipopata uhuru, wataalamu wamekuwa wakiweka mikakati ya kuangamiza umaskini, ujinga na maradhi lakini huwa hakuna nia ya kisiasa ya kuinua maisha ya wananchi. Mipango mingi imevurugwa na ufisadi na kuacha Wakenya wakiteseka huku wanasiasa na washirika wao wakiendelea kutajirika,” asema Bw Swaleh.

Anatoa mfano wa mpango wa laptopu ambao serikali ya Rais Kenyatta iliahidi wanafunzi mnamo 2013, na mpango wa afya kwa wote ambayo imebaki kuwa ahadi hewa.

“Ukweli ni kwamba watoto wa wanasiasa na matajiri wanasomea shule nzuri za kibinafsi ambako wana vifaa bora vya masomo, huku wale wa maskini wakitaabika kwa misongamano madarasani na ukosefu wa vifaa. Kuwanyima maskini elimu bora ni kuwanyima utajiri. Tangu uhuru vita dhidi ya umaskini, ujinga na magonjwa vimekuwa vya ubaguzi,” asema Bw Swaleh.

Serikali imejenga shule nyingi, vyuo na hospitali tangu uhuru lakini gharama ya elimu na huduma za matibabu ingali ya juu huku wanafunzi kutoka familia maskini wakikatiza masomo kwa sababu ya kukosa karo. Hii ni licha ya serikali kutangaza kuwa kuna elimu bila malipo.

Wadadisi wanasema licha ya Serikali kujenga shule nyingi kuliko ilivyokuwa wakati Kenya ilipopata madaraka ya kujitawala, zaidi ya thuluthi moja ya vijana wanaosoma hadi vyuo vikuu hawana kazi, huku chache zinazopatikana zikipewa walio watoto wa matajiri.

Sensa ya mwaka jana ilionyesha kuwa vijana milioni 5 hawana ajira, hali inayoongeza pengo kati ya matajiri na maskini.

Wataalamu wanasema inasikitisha kuwa miaka 57 baada ya Kenya kupata madaraka, bado kuna watu wasioweza kumudu gharama ya matibabu, wanakosa chakula na makao ilhali serikali imekuwa ikitengea sekta hizi mabilioni ya pesa kila mwaka.

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya uchumi Humphrey Were, kama serikali ingekuwa ikitekeleza mikakati ya uchumi inayowekwa na wataalamu, viwango vya umaskini vingekuwa vimepungua pakubwa.

“Inasikitisha mitaa ya mabanda inaendelea kuongezeka na maskwota wanazidi kuwa wengi miaka 57 baada ya uhuru. Maadui wale wale ambao waanzilishi wa taifa hili waliahidi kuangamiza 1963 bado yanaangamiza Wakenya hadi sasa hasa umaskini na maradhi,” asema.

Mtaalamu huyo anaongeza kuwa serikali zinazoingia mamlakani huwa haziweki mazingira ya kupigana na umaskini na maradhi.

Kulingana na Dkt Judith Ndiku wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro, umaskini unatatiza azima ya watu wengi maishani.

“Umasikini unaumiza wengi. Kutojua kusoma bado ni changamoto na maradhi yangali yanaua wengi,” Dkt Ndiku anasema.

Anaeleza kwa sababu ya umasikini, asilimia 56 ya Wakenya hawapati huduma za kimsingi.

“Juhudi za kumaliza umaskini nchini Kenya zimo tu kwenye ripoti za wataalamu, tume na mipango ya maendeleo. Hata hivyo, utekelezaji umebaki tatizo kubwa,” asema.