Miguna aapa kurudi Kenya kwa lazima
Na CHRIS WAMALWA na BENSON MATHEKA
Kwa Muhtasari:
- Miguna asema hata Rais Uhuru Kenyatta hawezi kumzuia kurudi Kenya kuendelea kutetea haki za uchaguzi
- Asema atarejea nchini haraka itakavyowezekana
- Aitaka jamii ya kimataifa kuongeza shinikizo kwa serikali ya Kenya kuheshimu utawala wa kisheria na uhuru wa wanahabari
MWANASIASA mbishi Miguna Miguna, ambaye wiki iliyopita alifukuzwa Kenya na kurudishwa Canada kwa kuhusika katika kiapo cha kinara wa NASA Raila Odinga, amesema anapanga kurudi Kenya hivi karibuni licha ya serikali kumpiga marufuku.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo katika ofisi za kampuni yake ya uwakili jijini Toronto, Canada mwishoni mwa wiki, wakili huyo aliyejitangaza jenerali wa vuguvuvu lililoharamishwa la National Resistance Movement (NRM), alisema hata Rais Uhuru Kenyatta hawezi kumzuia kurudi Kenya kuendelea kutetea haki katika uchaguzi.
“Nimepokea ripoti kuwa Uhuru Kenyatta na William Ruto wanasema haijalishi idadi ya maagizo nitakayopata. Hata nipate maagizo milioni moja hawataniruhusu kuingia Kenya tena. Ujumbe wangu kwa Uhuru Kenyatta na William Ruto ni huu; Kenya sio mali yenu na nitarudi. Samahani,” alisema.
Haraka iwezekanavyo
Alipoulizwa ni lini anafikiria kurudi nyumbani, Bw Miguna alisema: “Haraka itakavyowezekana. Ninajua mke wangu hatafurahi kusikia hayo lakini unafaa kuamua unavyotaka kuishi maisha yako na kumbukumbu unayotaka kuacha.
Tunavyoongea sasa, mawakili wangu wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu wakiomba unaodaiwa kuwa uamuzi wa kunipokonya uraia ubatilishwe,” alisema Bw Miguna.
Ilipomfurusha, serikali ya Kenya ilisema hakuwa Mkenya na kwamba hakufuata sheria kupata paspoti yake ya Kenya. Alikamatwa na kuzuiliwa kwa siku tano kufuatia hatua aliyotekeleza katika kiapo ambacho Bw Odinga alikula Januari 30 kuwa Rais wa Wananchi.
Mapuuza kuhusu demokrasia
Bw Miguna aliitaka jamii ya kimataifa kuongeza shinikizo kwa serikali ya Kenya kuheshimu utawala wa kisheria na uhuru wa wanahabari akisema serikali za nchi za bara Ulaya na Amerika hujifanya kutetea demokrasia, uwazi na uhuru wa wanahabari lakini wanapuuza umuhimu wa masuala hayo Afrika na nchi zinazoendelea.
“Hizi serikali zinazoitwa zilizoendelea, zinafaa kufanya zaidi ya kuliko maneno tu kuhusu mambo haya,” alisema Bw Miguna.
Alisema yaliyompata mikononi mwa serikali yanafaa kuwagutusha Wakenya wanaoishi ng’ambo ili wafuatilie yanayoendelea nyumbani. Alisema ujumbe wake kwa Wakenya walio ng’ambo ni kuungana na kutokuwa na woga.
“Eleweni kwamba Kenya ni yetu sisi sote,” alisema.