HabariSiasa

'Miguna atarejea Kenya baada ya matibabu nchini Canada'

April 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAKILI mtatanishi Miguna Miguna amewasili jijini Toronto, Canada, Jumatatu baada ya kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai ambako aliishi kwa siku nne kufuatia kuzuiwa kuingia nchini.

Mmoja wa mawakili wake, Nelson Havi, Jumatatu alisema Dkt Miguna aliondoka Dubai, kwa hiari yake, kwa usaidizi wa ubalozi wa Canada nchini Muungano wa Milki za Kiarabu (UAE).

“Alisafiri hadi Toronto, Canada. Atapokea uchunguzi wa kubaini aina ya sumu ilitumiwa kumdunga ili apoteze ufahamu kusudi asafirishwe kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na kusafirishwa hadi Dubai. Atarejea Kenya baada ya kupata matibabu,” Bw Havi akaandika kwenye ukurasa wake wa twitter.

Kulingana na afisa mmoja wa cheo cha juu serikali Dkt Miguna alisafiri kwa ndege moja ya shirika la Air Canada 57 (ACA57) baada ya kuonyeshana paspoti yake ya Canada, ambayo alidai kuwa ilipotea wakat wa kizaazaa katika JKIA, Nairobi.

“Maafisa wa UAE wameanzisha uchunguzi kubaini jinsi ambavyo alipata paspoti yake ya Canada ambayo alifeli kuwapa maafisa husika alipoondoka Kenya na kuwasili Dubai,” afisa wa UAE ambaye hakutaka kutambuliwa alisema Jumatatu.

“Kenya pia ingependa kuchunguza jinsi Miguna alirejeshewa paspoti baada ya kuwakashifu maafisa wa serikali wa Kenya akidai kuwa ndio walimpokonya kwenye vuta nikuvute iliyotokea katika JKIA,” akaongeza.

Mitambo ya kutambua ndege ilionyesha kuwa ndege hiyo iliyombeba Dkt Miguna aliondoka Uwanja wa Ndege wa Dubai lango nambari D21 Jumapili mwendo wa saa tano na dakika 58 za usiku, saa za UAE.

Na ikatua katika Uwanja wa Kimataifa wa Toronto Pearson saa kumi na moja na dakika 14 saa za Canada na saa sita na robo (12.15pm) saa za Kenya baada ya safari ya saa 13 na dakika 25.

Dkt Miguna ambaye aliwasili Dubai mnamo Alhamisi asubuhi, alikaa nchini UAE kwa siku nne akipokea matibabu.

 

‘Sumu’

Alikuwa amelalamika kuugua kutokana na kile alichodai ni hatua ya maafisa wa polisi wa Kenya kumdunga kwa kemikali yenye sumu ili mwili wake ukafa ganzi na ndipo watamsafirisha hadi Dubai.

Alitibiwa katika Hospitali ta Sheikh Rashid iliyoko jijini Dubai kisha akaruhusiwa kuondoka.

Wakili huyo ambaye hujitambua kuwa jenerali wa kundi uasi lilipigwa marufuku la Nationala Resitance Movement (NRM) alifurushwa kutoka nchini Kenya mnamo Machi 28, baada ya makabiliano na maafisa wa usalama na idara ya uhamiaji kwa saa 72.

Alitaka aruhusiwe kuingia nchini Kenya bila kuwasilisha paspoti ya Canada aliyotumia kusafiria, akidai mahakama iliamuru aingia nchini bila masharti yoyote.

Vile vile, alikataa kutia saini stakabadhi za uhamiaji ili aruhusiwe kuingia nchini huko utata kuhusu paspoti yake ya Kenya ukishughulikiwa.

Wakili Miguna kwanza alifurushwa nchini mnamo Februari 9 baada ya serikali kudai kuwa alikuwa amekana uraia wake wa Kenya na kupata uraia wa Canada mnamo 1998.

Maafisa wa idara ya uhamiaji walidai kuwa tangu wakati huo Dkt Miguna hakuwahi kuwasilisha ombi la kutaka arejeshewe uraia wake wa Kenya.