Mikakati ya Ruto kuingia Ikulu
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto yumo mbioni kuweka mikakati kabambe ya kuimarisha nafasi yake ya kuingia Ikulu 2022 licha ya Rais Uhuru Kenyatta kuonya wanasiasa dhidi ya kuanza kampeni za mapema.
Kwanza, Dkt Ruto anajinadi kwa raia kupitia ziara za kila mara maeneo mbalimbali nchini ‘kuzindua miradi ya maendeleo’, kuchanga fedha za kusaidia makanisa, shule na makundi ya kijamii na pia kuhudhuria mazishi.
Anatetea ziara hizi, akazitaja kama za kimandeleo na anazofanya “kwa niaba ya Rais Kenyatta” kwa ajili ya kuvumisha Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee.
“Kwa sababu mimi ndiye mtu wa mkono wa Rais, sharti nitembee kila mahali nchini kukagua miradi ya serikali ili kuhakikisha inakamilishwa ilivyopangwa. Nitahakikisha manifesto ya Jubilee inatekelezwa kote nchini ili kuhakikisha Rais anaacha sifa nzuri,” Dkt Ruto akasema mapema Agosti alipoongoza mchango wa fedha katika kanisa Katoliki la St Mary, eneobunge la Kiharu, Murang’a.
Katika muda wa siku saba zilizopita, amehudhuria hafla mbalimbali katika kaunti za Narok, Kakamega, Nairobi, Kericho na Meru huku akiandamana na viongozi wa kisiasa wanaounga mkono azma yake ya kuingia Ikulu.
Kwa mfano, mnamo Jumamosi pekee, Dkt Ruto alihudhuria hafla ya mazishi ya mwanajeshi wa Amerika marehemu Chris Atema ambaye ni mwanawe Mbunge wa Ikolomani Benard Shinali katika kaunti ya Kakamega na mashindano ya michezo baina ya kaunti katika uwanja wa michezo wa Kericho Green Stadium.
“Mkakati huu wa kuzuru sehemu mbalimbali nchini, unamfaa zaidi Naibu Rais katika azma yake ya kugombea urais 2022 kwa sababu unamwezesha kuonekana na wananchi kupitia harambee na mikutano mingineyo,” asema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Martin Andati.
Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Dkt Boni Khalwale anaungama Dkt Ruto husaidia makanisa kupitia michango ya fedha kwa sababu “huko ndiko kuna watu wengi.”
“Takribani asilimia 80 ya Wakenya ni Wakristo. Kwa hivyo, kwa kusaidia miradi ya Kanisa kupitia michango ya fedha, Dkt Ruto anadhihirisha kuwa yeye ni kiongozi anayejali sehemu kubwa ya raia wa nchi hii,” anasema.
Kauli yake inaungwa mkono na Mbunge wa Soy Caleb Kositany anayemtaja Ruto kama “kiongozi mcha Mungu.’
Inaaminika kuwa Dkt Ruto pia ndiye mdhamini wa kundi la viongozi wanawake, ‘Inua Mama’ ambao wamekuwa wakizunguka kote nchini kuvumisha azma yake ya kuingia Ikulu 2022.
Kundi hilo la wabunge wanawake limekuwa likimsuta kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye anaonekana kuwa kizingiti kikuu kwa azma ya Dkt Ruto kuwa rais.
Wadadisi wanasema Naibu Rais alianza kujipanga kwa safari ya Ikulu baada ya Jubilee kushinda uchaguzi mkuu wa 2017 kwa kuweka mikakati ya kudhibiti bunge la kitaifa na Seneti. Alifanya hivyo kwa kuhakikisha wandani wake ndio wanateuliwa kuwa katika safu ya uongozi wa bunge.
“Mkakati huo ndio ulimwezesha Aden Duale (Mbunge wa Garissa Mjini) kuhifadhi cheo cha kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa na Benjamin Washiali (Mbunge Mumias Mashariki) kuteuliwa kiranja.”
“Na katika seneti, alihakikisha Kipchumba Murkomen (Seneta wa Elgeyo Marakwet) anateuliwa kiongozi wa wengi huku Susan Kihika (Seneta wa Nakuru akiteuliwa kiranja wa wengi,” anasema Tom Mboya.
Anasema viongozi hawa watakuwa na ushawishi mkubwa zaidi wakati wa uchaguzi wa Jubilee utakaofanyika Machi mwaka ujao.
Dkt Ruto pia amekuwa akikutana na madiwani wa Jubilee nyumbani kwake Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu katika kile kinachoonekana kama hatua ya kujipanga kwa uchaguzi wa Jubilee na mchujo wa mgombea urais.
“Hali hiyo, bila shaka itaboresha nafasi ya Dkt Ruto kushinda wakati wa mchujo wa mpeperushaji bendera katika uchaguzi mkuu wa 2022,” asema Dkt Mboya ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maseno.
Katiba
Kuhusu mjadala wa mabadiliko ya Katiba kupitia kura ya maamuzi ambao umeshika kasi wakati huu, Dkt Ruto anaonekana kuegemea mpango ambao utadumisha mamlaka ya sasa ya Rais.
Wandani wake wanaunga baadhi ya mapendekezo kwenye mswada wa “Punguza Mizigo” ambao pia unashabikiwa na madiwani wengi na ambao inadaiwa anadhamini.
Kwa upande mwingine, wanapinga jopokazi la maridhiano (BBI) linaloungwa mkono na wanasiasa wanaopendekeza kupanuliwa kwa ngazi ya uongozi kupitia kubuniwa kwa vyeo vya waziri mkuu na manaibu wake wawili.
Naibu Rais Dkt Ruto pia amewkeza katika sekta ya uanahabari, baada ya kununua hisa katika gazeti moja la kila siku.
Vile vile, duru zasema amenunua redio za lugha za kiasili na kituo kimoja cha runinga, ili kusaidia kuvumisha sera zake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.
Lakini mbinu kuu zaidi anayotumia kwa sasa, ambayo wadadisi wasema inaweza kuwa msumeno-imfae au imdhuru kisiasa ni kujisawiri kama ‘hasla’, mwanasiasa mlalahoi ambaye amekwea jukwaa la uongozi kutokana na bidii yake ya mchwa.
Ataka kinyang’anyiro cha 2022 kionekane kama kwamba ni kati ya wale viongozi kutoka nasaba bora na wale maskini ambao wameingia kwenye meza ya wakubwa kutokana na weledi na ukakamavu wao.
Hata hivyo, wengi wamemhusisha na madai ya kashfa nyingi za uporaji wa fedha za umma. Pia, historia yake kama mwanachama wa kundi la Youth for Kanu 1992 lililompigia debe Rais Mstaafu Daniel Moi ambapo uchumi wa nchi ulisambaratika kabisa huenda ikamponza.