MIMBA ZA MAPEMA: Jinsi 'usasa' ulivyoharibu makuza mema
Na MISHI GONGO
JUNI 2020 Wakenya walikumbwa na hali ya wásiwasi kufuatia nchi kuandikisha idadi kubwa ya matineja kupata mimba.
Maswali yaliyogonga vichwa vya wengi ni nani wa kulaumiwa kutokana na hali hiyo.
Mtafiti wa mila na tamaduni za Kiswahili eneo la Pwani Bi Hamira Saidi analaumu hatua ya watu kuacha mila na kuingilia usasa usasambu kama chanzo cha kudorora kwa maadili.
Kulingana na mtafiti huyo, jamii imeacha kufuata mila na tamaduni zake na kufuata uzungu.
Akizungumza na Taifa Leo Ijumaa, alitaja mavazi ovyo, na watoto kutokanywa kama sababu zinazochangia katika tatizo la mimba za mapema.
“Zamani mtoto wa kike aliyevunja ungo hakuruhusiwa kujipamba kupitiliza na alishajiishwa avalie nguo za heshima muda wote. Sasa hivi unapotembea barabarani ni kawaida kuona mabinti wakitembea nusu uchi wakiwa wamejikwatua,” akaeleza.
Bi Saudi alieleza kuwa vipodozi huwafanya rijali kuchemkwa na damu na kuanza kuwaandama mabinti.
Alisema hali hiyo huwafanya wasichana kuangukia katika mikono ya mabarobaro wasio na nidhamu ambao huwahadaa na kuwapachika mimba.
Aidha alisema mabinti pia hawakuruhusiwa kutangamana na vijana wa kiume. Wazazi nao walijitahidi kuwapa watoto malezi bora kinyume na sasa.
Alieleza kuwa pindi tu msichana alipovunja ungo, alipelekwa kwa somo; mwanamke ambaye alimfunza majukumu yake katika jamii na madhara ya kujihusisha katika ngono kabla ya ndoa.
Hata hivyo alisema mila hiyo haitekelezwi tena kwa sasa.
“Nyakati tulizo nazo, wazazi hawana sauti ndani ya nyumba; yaani watoto leo hii wanafanyiwa wanachokitaka,” akasikitika.
Alitaja mabinti kuangalia filamu chafu miongoni mwa vitu vinavyowasukuma kuingilia ngono za mapema.
“Katambo ilikuwa ni mwiko kwa mtoto wa kike kuvaa nguo inayomuonyesha babake mapaja, lakini sasa utamwona binti amevaa sketi au kinyasa kifupi akiwa ameketi sebuleni na babake ambaye pia ana kinyasa bila shati wakitizama filamu zenye picha za ngono au vijisehemu vya mahaba. Hali hii inachangia ongezeko la mabinti kunajisiwa na kubakwa na jamaa zao wa karibu,” akasema.
Alisema watoto wanapobalehe huhitaji kufuatiliwa kwa karibu na kupewa ushauri nasaha wa kuwa vielelezo bora katika jamii.
Hata hivyo alisema wazazi wengi hulegeza kamba pindi tu mtoto anapobalehe na kumuacha afanye anachotaka.