RAIS William Ruto anapanga kutumia zaidi ya nusu ya bajeti ijayo kwa miradi yake ya kipaumbele ikiwemo makazi, elimu, afya na miundombinu, inavyoonyesha rasimu ya Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS) kwa mwaka wa kifedha 2026/27.

Wizara ya Fedha imetenga Sh1.66 trilioni kwa sekta hizi nne katika bajeti ya jumla ya Sh2.88 trilioni kwa mwaka wa kifedha unaoanza Julai 1, 2025.

Kulingana na rasimu hiyo, sekta ya Afya imetengewa Sh167.4 bilioni, ikijumuisha Sh136 bilioni kwa matumizi ya kawaida na Sh31.4 bilioni kwa maendeleo.

Sekta ya Elimu itapokea Sh767.3 bilioni, ambapo Sh737.2 bilioni ni kwa matumizi ya kawaida na Sh30.1 bilioni kwa maendeleo.Sekta za Kawi, Miundombinu na ICT zimetengewa Sh194.5 bilioni, ikijumuisha Sh151.6 bilioni kwa matumizi ya kawaida na Sh42.3 bilioni kwa maendeleo.

Sekta ya Makazi, inayolenga kutimiza ahadi ya kampeni ya Ruto ya makazi ya bei nafuu, imetengewa Sh139.3 bilioni, ikiwemo Sh133.6 bilioni kwa maendeleo ya makazi na Sh5.7 bilioni kwa matumizi ya kawaida.

Katika sekta ya Afya, serikali imepanga kuajiri wahudumu wa Afya wa Jamii (na kusajili Wakenya 35 milioni katika Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).

Hadi sasa, Wakenya zaidi ya 27 milioni tayari wamesajiliwa, ikiwakilisha ongezeko la zaidi ya asilimia 200 kutoka milioni 9 waliokuwa chini ya NHIF, na zaidi ya 21 milioni wakiwa wanachangiaji wapya kabisa.

“Serikali inapanga kukamilisha usajili wa Wakenya wote wanaostahili katika SHA, kwa lengo la kufikia watu 35 milioni,” inasema rasimu ya BPS.

Miradi ya miundombinu ya afya ni pamoja na ujenzi wa vituo vipya vya afya, kukarabati na kuweka vifaa vya kisasa katika vituo vilivyopo, na ukarabati wa hospitali.

Pia, serikali imeanzisha mitandao 228 ya Afya ya Msingi nchini kote na kuajiri wahudumu wa afya wa jamii 120,000 watakaopokea mishahara ya kila mwezi.

Kwenye mpango wa Makazi ya Bei Nafuu (AHP pia, masoko 506 yatajengwa kusaidia shughuli za kiuchumi.

Serikali pia inalenga kuendeleza miji na mipango ya upanuzi wa miji ili kupunguza msongamano katika miji mikubwa na kuunda jamii zenye mpangilio mzuri na miundombinu ya pamoja.

Wizara pia itapanua ufadhili wa Hazina ya Makazi kwa kupanua Boma Yangu na kutoa mikopo ya kupata makazi vijijini.

Katika sekta ya elimu, serikali inalenga kukuza masomo ya ufundi na elimu ya msingi kwa kuajiri walimu 30,000 zaidi, kujenga madarasa 20,000 mapya na kukarabati madarasa 15,000, pamoja na kufanikisha mafunzo ya walimu 50,000 kwa mbinu za elimu ya umilisi.

Sekta ya miundombinu pia inajumuisha ujenzi wa mabwawa, barabara na kuongeza uwezo wa umeme kwa megawati 10,000 kupitia miradi ya nguvu za mvuke, jua, upepo na umeme wa maji.

Serikali inaashiria kuwa miradi hii yote itasaidia kuunganisha vituo vikuu vya uchumi, kuimarisha uchukuzi vijijini, kukuza kilimo na kuendeleza uchumi wa viwanda.